1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: CUF yamchagua tena mwenyekiti wake Lipumba

19 Desemba 2024

Chama cha wananchi CUF cha nchini Tanzania kimeendelea kumweka kwenye safu yake ya uongozi mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba aliyechaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka mitano ijayo.

Ibrahim Lupumba, CUF
Lipumba anaweka rekodi kwa kuwa mwenyikiti aliyehudumu kwa kipindi kirefu zaidi Picha: Said Khamis/DW

Lipumba ambaye anaweka rekodi kwa kuwa mwenyikiti wa sasa kwa kipindi kirefu zaidi anakabiliwa na jukumu la kurejesha ushawishi wa chama hicho wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu hapo mwakani. 

Ni tambo na vijembe ambavyo mara nyingi Profesa Lipumba amekuwa akivihanikiza wakati anapopanda katika majukwaa ya kisaasa vikielelezwa kwa chama tawala CCM na sera zake.

Soma pia: Lipumba aitaka serikali kuionya Urusi kuhusu kundi la Wagner

Mwanasiasa huyo ambaye amepata kugombea nafasi ya urais zaidi ya mara tatu, amechaguliwa kuongoza tena chama hicho cha upinzani katika mkutano mkuu uliomalizika jana usiku, akiwashinda wapinzani wake kwa idadi ndogo ya kura. Matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho Mashaka Ngole, yalionyesha kuwa Lipumba ametetea nafasi yake kwa kuondoka na kura 216, wakati aliyemfuatia Hamad Masoud akijikusanyia jumla ya kura 181.

Ushindi wake mwembamba dhidi ya aliyekuwa makamu wake uanashiria namna mwanasiasa huyo anavyokabiliwa na mtihani wa kimahesabu ndani ya chama na kwamba huenda atalazimika kuzikagua upya sera zake kelekea katika kipindi chake cha miaka mitano ijayo.

Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama cha upinzani CHADEMA akiwa na Ibrahim Lipumba wa chama cha CUFPicha: Ericky Boniphace/DW

Soma pia: CUF yapinga vikali kuibuka kwa pendekezo jipya kuhusu katiba

Lipumba anaendelea kusalia katika uongozi wa chama katika wakati ambapo ushawishi wa chama hicho ukiendelea kuporomoko na kuzua wasiwasi juu ya majaliwa ya chama chenyewe wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani.

Cuf ambayo miongo kadhaa iliyopita ilizitawala siasa za upinzani kuanzia visiwani Zanzibar mpaka bara, sasa siyo tishio tena katika medani za siasa, na kulingana na baadhi ya wachambuzi wa mambo kiongozi huyo inaweza ikawa ni sehemu ya sababu ya kuanguka kwa chama hicho.

Mwandishi wa habari wa siku nyingi na ambaye pia wakati mmoja amewahi kuwa mbunge, Said Kubenea anasema Lipumba hakupaswa kugombea tena katika kinyang'anyiro hicho na kwamba haiba yake ilidorora tangu alipokikacha chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baadaye kuamua kurejea tena.

Hata hivyo, chama hicho bado kimebakiza ushawishi wake katika baadhi ya maeneo ikiwamo maeneo ya pwani ya kusini. Wakati baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa katika mchaka mchaka wa uchaguzi wa ndani vikijipanga kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Chama kingine cha upinzani Chadema kinatarajiwa kufanya uchaguzi wake Januari 22 huku macho ya wafuatiliaji wa mambo yakiekekezwa kujua nani atakuwa kinara wa chama katika nafasi ya uenyekiti.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW