1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania haina mpango wa kuikubali chanjo ya corona

2 Februari 2021

Wizara ya afya nchini Tanzania imesema haina mpango wa kukubali chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid 19, siku chache tu baada ya Rais John Magufuli kutilia mashaka juu ya chanjo hiyo bila ya kutoa ushahidi.

Tansania Dar es Salaam | Grafitty zu Corona
Picha: Eric Boniphace/DW

Kwengineko timu ya wachunguzi wakiongozwa na wataalamu kutoka shirika la afya duniani WHO wamewasili katika kituo cha wanyama katika mji wa kibiashara wa Wuhan, China ili kutafuta majibu juu ya chimbuko la virusi vya Corona. 

Waziri wa afya wa Tanzania Dorothy Gwajima aliuambia mkutano na waandishi habari katika mji mkuu wa Dodoma jana Jumatatu kuwa wizara hiyo haina mpango wowote wa kupokea chanjo dhidi ya virusi vya Corona. Amesema chanjo yoyote lazima kwanza iidhinishwe na wizara hiyo. Hata hivyo haijabainika wazi ni lini chanjo hiyo itafika nchini humo, licha ya kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yako chini ya mpango wa kimataifa wa kupokea chanjo COVAX, mpango ambao unalenga kutoa dozi hizo kwa mataifa maskini na yenye kipato cha kati.

Watalaamu wa WHO wako Wuhan, ChinaPicha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Waziri Gwajima amesisitiza kuwa Tanzania iko salama. Katika mkutano huo na waandishi wa habari, yeye pamoja na wengine waliohudhuria mkutano huo hawakuvaa barakoa japo amewatolea wito umma kudumisha usafi ikiwa ni pamoja na matumizi ya vitakasa mikono na hata pia kujifukiza. Hata hivyo, wataalamu wa afya wamepuzilia mbali mbinu hiyo ya kujifukiza au "kupiga nyungu” na kuitaja kuwa haina uwezo wa kuua virusi vya Corona.

Vile vile mkemia Mkuu wa serikali Fidelice Mafumiko amependekeza utumiaji wa dawa za mitishamba kutibu ugonjwa wa Covid 19 japo bila kutoa ushahidi. Serikali ya Tanzania imekosolewa vikali kwa jinsi ilivyofumbia macho janga la virusi vya Corona. Wizara ya afya haijatoa takwimu za watu wanaougua ugonjwa huo tangu Aprili mwaka uliopita, wakati maambukizi yalikuwa 509 wakati huo.

Wiki iliyopita, Mkuu wa shirika la afya duniani barani Afrika aliitolea mwito Tanzania kuweka wazi takwimu zake za ugonjwa wa Covid 19 huku naye mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika, John  Nkasonga akisema lazima kuwe na juhudi za pamoja barani Afrika za kupambana na janga la virusi vya Corona la sivyo huenda watu wengi wakaangamia.

Wakati hayo yanaarifiwa, Uingereza inaanza zoezi la upimaji wa nyumba hadi nyumba kwa watu 80,000 katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha Corona kilichogunduliwa Afrika Kusini.

Uingereza yaimarisha upimaji wa raia wakePicha: picture-alliance/AP Photo/J. Cairns

Wizara ya afya nchini humo imesema imetambua jumla ya maambukizi 105 ya aina mpya ya kirusi cha Corona tangu mnamo Disemba 22 na ili kuzuia maambukizi zaidi, wakaazi katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo sasa watalazimika kupimwa bila kujali iwapo wameonyesha dalili au la.

Upimaji huo unafanyika katika wakati ambapo idadi ya maambukizo nchini Uingereza inaendelea kupungua. Tayari Uingereza imeanzisha mpango wa chanjo huku kiasi watu milioni 9.3 wakipokea dozi ya kwanza ya chanjo.

Hata hivyo, kumeibuka wasiwasi kuwa aina mpya ya kirusi cha Corona huenda kikatia doa mafanikio waliopata katika kudhibiti janga hilo la ulimwengu.

Ama kwa upande mwengine, timu ya wachunguzi wakiongozwa na wataalamu kutoka shirika la afya duniani WHO wamewasili katika kituo cha wanyama katika mji wa kibiashara wa Wuhan ili kusaka majibu ya chimbuko la virusi vya Corona.

Timu hiyo tayari imetembelea hospitali kadhaa, na soko la wanyama la Huanan ambako kunaaminika kugunduliwa kisa cha kwanza cha virusi vya Corona.