Tanzania imetangaza rasmi kufuta hadhi ya ukimbizi
17 Oktoba 2025
Tangazo hilo limetolewa na mkurugenzi wa idara ya wakimbizi nchini Tanzania Sudi Mwakibasi siku ya Alhamisi katika ziara maalumu kwenye kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta. Ambako amefuatana na Viongozi kadhaa akiwemo mkuu wa mkoa IGP mstaafu Balozi Simon Sirro, mwakilishi wa UNHCR Tanzania, Balozi mdogo wa Burundi mkoani Kigoma na wakuu wa mashirika yanayohudumia wakimbizi
Akihutubia katika mikutano miwili mikubwa ya wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu mapema jana pamoja na mchana huu katika Kambi ya Nduta mkurugenzi huyo wa idara ya wakimbizi nchini Tanzania Sudi Mwakibasi amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuishi ukimbizini wakati nchi ya Burundi ina amani
Amesema "Serikali katika vikao vya kikanda na kitaifa muda wote iliomba kuungwa mkono kufuta hadhi ya wakimbizi kutoka Burundi kwa kuwa hakuna sababu za ukimbizi wao kwa sasa. Na katika kutambua jitihada za serikali ya Burundi kuleta amani na utulivu kwenye nchi hiyo jumuiya ya kimataifa pia iliiondolea Burundi vikwazo vya kiuchumi ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuridhishwa na hatua ambazo zimeendelea kuchukuliwa na Burundi."
Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma Inspekta Jenerali wa polisi na Balozi mstaafu Simon Siro ameeleza kuwa kufuatia matokeo ya dodoso na hojaji za wakimbizi wote imebainika kuwa wakimbizi kutoka Burundi hawana sababu ya kutorejea nchini mwao. "Tusitegemee vitu vya kupewa, lazima tuijenge Afrika yetu. Tusiwe watu wa kuombaomba kila wakati. Afrika yetu itajengwa na sisi Waafrika wenyewe...."
Balozi mdogo wa Burundi anayehudumia mkoa wa Kigoma Jeremiah Kekenwa anathibitia kuwa Burundi ni nchi yenye usalama wa kutosha.
Mwakilishi mkazi wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Tanzania Barbara Bentum amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono mipango ya kuwarudisha wakimbizi hao nchini mwao ampapo wakimbizi elfu tatu watakuwa wakirudi burundi kila wiki kuanzia sasa na amewahimiza wakimbizi kujitokeza na kujiorodhesha kwa ajili ya kurejea nyumbani.