1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TANZANIA INAENDELEA KUTUMIKA KAMA NJIA KUU YA WAHAMIAJI HARAMU

Christopher Buke16 Agosti 2006

Ni wale wanaokwenda Ulaya, Marekani na Afrika Kusini

Tanzania inaendelea kutumiwa na wahamiaji haramu wanaokimbilia barani Ulaya, Marekani na Afrika Kusini huku Wataalamu wakiendelea kuonya kuwa hali hiyo isipodhibitiwa tatizo hili litazidi kuongezeka kila uchao.

Akizungumza na waandishi wa habari July 28, mwaka huu wa 2006, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Action for Development Forward (AFDF), Bwana Renatus Mkinga alidai kuwa hivi sasa wahamiaji hao wana mtandao mkubwa.

Alikosoa lawama zinazotolewa dhidi ya Idara ya Uhamiaji nchini kuwa imeshindwa kudhibiti tatizo la wahamiaji haramu.

Matokeo ya kura za maoni ambayo yaliendeshwa na Kituo cha Televesheni nchini Tanzania cha ITV yalionyesha kuwa asilimia 70 ya washiriki katika maoni hayo walidai kuwa Idara ya Uhamiaji imeshindwa kudhibiti wageni haramu wanaoishi nchini na wengine kupewa vibali kufanya kazi hata zile ambazo zingeweza kufanywa na wananchi wazawa.

Bwana Mkinga anadai kuwa wageni halali wakiwemo wawekezaji, watalii, wanafunzi nk. , wanaoingia Tanzania wanakuja kwa mujibu wa sheria na wala sio kazi ya Idara ya Uhamiaji kuzuia wageni bali kuhakikisha wanaingia kisheria.

Kwa mujibu wa maelezo ya mkurugenzi huyo, licha ya kuwa kuna kundi la wahamiaji haramu wanaoingia Tanzania ili kuishi au kuitumia nchi hii kama njia ya kwenda nchi nyingine, wengine huingia kufanya biashara bila kufuata taratibu za kisheria, lakini wengine wakikimbia vita na mapigano katika nchi zao au mbinyo wa kisiasa hasa katika nchi za Rwanda, Burundi DRC Somalia nk.

Anataja sababu nyingine kuwa, kutokana na rasilmali nyingi ilizonazo Tanzania baadhi huja kwa nia ya kupora au kuendesha biashara zao kwa kukwepa ushuru.

Anasisitiza kuwa nchi hii ina akiba kubwa ya madini na kuwa katika kilomita za eneo la mraba 960,000 za ardhi ya Tanzania 850,000 zina madini mbalimbali kama dhahabu almasi platinum, cobalt, tanzanie, madini ya rubi na mengine mengi.

Anaendelea kudai kuwa mengi ya madini haya yamekuwa yakitoroshwa nje bila kulipiwa alau ushuru na kuwa njama hizo hufana kutokana na sababu mbalimbali moja wapo ikiwa ni njia nyingi za panya zilizomo kwenye mipaka ya Tanzania na nchi jirani.

Njia nyingine anayodai inasaidia kutoroshwa kwa madini ya Tanzania ni kutokana na tatizo la ubadhilifu na rushwa kwa baaadhi ya vingozi au hata wananchi wa Tanzania.

Anakosoa mfumo ulio kwenye mikapa ya Tanzania na majirani zake hivi sasa, hauwezi kufanya chochote cha kuwadhibiti wahamiaji haramu wala wavukao mpaka kwa nia mbanya isipokuwa kuwarahisisa kazi hiyo.

Anatoa mfano wa hali ya mipaka mingi haijatengwa ili iachwe sehemu muhimu kama ilivyo sheria ya mipaka inayotaka liachwe eneo la wazi lisilomilikiwa na mtu No man’s land hasa katika mipaka ya Tunduma, Namanga, Holili, Tarakeoa, Mtukura na Sirali.

Tatizo lingine linalotajwa na Bwana Mkinga ni vitendea kazi vya kutosha na vya kisasa pamoja na wafanyakazi man power. Bila ya hivyo anasisitiza kuwa itakuwa vigumu kudhibiti mipaka ya Tanzania ya nchi kavu, bahari, mito na maziwa.

Kasoro nyingine anayoiona Bwana Mkinga inayoselelesha tatizo hili ni ubinafsishaji na sheria zake. Anadai wawekezaji na wageni wameruhusiwa kuendesha Idara nyeti bila kuzingatiwa umuhimu wake.

Kuthibitisha dai hili anatumia mfano wa hivi karibuni ambapo kontena lenye tani tatu za meno ya ndovu lilikamatwa katika bandari ya Singapore likiwa njiani kwenda katika nchini Ufilipino likitokea Tanzania.

Kontena hilo lilikuwa na nyaraka bandia kutoka makampuni ya kigeni ambayo yanafanya biashara ya uwakala na umiliki wa meli nchini.

Anasema hali hii itaendelea kujitokeza tofauti na ilivyokuwa zamani wakati ambapo mawakala wa kudhibiti mizigo kama hiyo katika bandari nchini lilikuwa ni shirila la NASACO.

Anaitetea Idara ya uhamiaji Tanzania kuwa sio inayoruhusu wawekezaji kuingiza watu na kuwaruhusu wafanye kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania, bali hii ni kwa mujibu wa maelekezo ya kituo cha uwekezaji Tanzania TIC.

Mathalan, anadai Bwana Mkinga wawekezaji nchini wanaruhusiwa kuingia na watu watano wawe ni wake zao au waume zao, awe mke, mtoto wake, au mjomba wake “hata kama hajui kusoma na kunandika anaruhusiwa kumuingiza nchini na kumuajiri sababu anachotaka mweekezaji sio madigirii au madiploma anachotaka yeye ni uaminifu na kwamba mali zake zimo katika mikono ya watu anaowaamini” anaongeza Bwana Mkinga.

Inakadiriwa kwamba Tanzania ina wageni wahamiaji milioni moja. Asilimia 90 kati ya hao ni wale walioingia kama wakimbizi.

Mkurugenzi huyo anaonya kuwa kutokana na utandawazi shinda na rushwa Mfumo wa ulinzi na usalama “ wa nchi yetu umekufa na watanzania sasa wamepoteza uzalendo wao kwani sasa ndio wanawaficha wageni na kuwasaidia kuishi nchini isivyo halali na wala hawatoi ushirikiano kwa Idara za uhamiaji, polisi nk.” anasema Bwana Renatus.

Anadai wakati wa vita vya Tanzania na Uganda miaka ya 1978-1979 “ wananchi wa mikoa ya Kaskazini walikuwa macho sana na wageni”.

“wakimuona mtu ambaye hawamfahamu mara moja walipiga ripoti sehem husika na huu ndio ulikuwa mfumo wa nchi nzima, watu walikuwa macho na ulinzi wa nchi yao, leo hii wageni kuingizwa hapo kiharamu ni biashara, wageni wanatoka Somalia wanasindikizwa na wakenya kupitia njia za panya halafu wanapokelewa na watanzania ambao hulipwa wastani wa dola 100 kwa kila mtu moja wakiwa na nia ya kuwasaidia kuvuka Tanzania kwenda Afrika kusini”.

Anasema baadhi ya wageni hao ambao wanaishi au kufikia kwenye nyumba za kulala wageni vitabu kwenye nyumba hizi havijazwi jinsi inavyopaswa lakini pia “umekuwa ni mtindo wa wamiliki wa hoteli hizo na nyumba za kulala wageni kuto orodhesha idadi kamili ya wapangaji kwa mijajili ya kukwepa kodi”.

Alipozungumza na waandishi wa habari May 5, 2006 Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Bwana Herbert Chilambo alidai kuwa kutokana na uhaba wa Wafanyakazi wa kutosha na zana za kisasa katika Idara yake wahamiaji haramu hasa kutoka nchi za Upembe wa Afrika wamekuwa wakiitumia Tanzania kama daraja la kwenda chini Afrika Kusini na kisha kwenda nchi za Ulaya na Marekani.

Mwisho.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW