1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania inafanya uchaguzi mkuu

28 Oktoba 2020

Watanzania wanapiga kura leo katika uchaguzi mkuu ambapo Rais John Magufuli anayekiongoza chama tawala cha CCM anatumai kushinda muhula mwingine wa miaka miaka mitano kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki.

Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu

Wapinzani wakuu wa Magufuli ni pamoja na Tundu Lissu wa chama cha Cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA na Bernard Membe wa chama cha ACT Wazalendo. Ni uchaguzi mkuu wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Hapo jana wakaazi wa visiwani Zanzibar walianza kupiga kura lakini awamu ya jana ilikuwa inahusisha makundi maalum.

Katika muda mfupi ujao vituo vya kupigia kura vitafunguliwa ambapo kwa mujibu wa maafisa wa uchaguzi, zoezi hilo litaendelea hadi saa kumi na mbili jioni kabla ya kuanza shughuli ya kuhesabu kura hizo. Zaidi ya watu milioni 30 wamesajiliwa kupiga kura kati ya raia milioni 58. Watamchagua rais kutoka kwa wagombea 15 na kuwachagua wawakilishi wao katika bunge lenye viti 264.

Magufuli mwenye umri wa miaka 60, anajinadi kwa kutaja miradi yake mikubwa ya maendeleo ya miundombinu na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi na ameitisha uchaguzi wa amani. "Kwa wale waliosajiliwa, pigeni kura na muende nyumbani. Iacheni tume ya uchaguzi ifanye kazi yake. Amani ni muhimu sana na naomba itawale katika uchaguzi huu," alisema jana.

Mpinzani mkuu wa Magufuli, Lissu mwenye umri wa miaka 52 alisema katika mkutano wake wa mwisho wa hadhara kuwa "Nimeshuhudia kupitia kampeni kuwa Watanzania wako tayari kwa mabadiliko na naamini kuwa watajitokeza na kupiga kura."

Katika upande wa Visiwani Zanzibar, mgombea wa upinzani Seif Sharif Hamad akiwa katika kinyang'anyiro chake cha sita cha urais mara hii akipeperusha bendera ya chama cha ACT Wazalendo, anapambana na mgombea wa CCM Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Zanzibar in historia ya mazingira tete ya uchaguzi yanayokumbwa na machafuko na makosa na upinzani kwa mara nyingine umekituhumu chama tawala cha CCM kwa kutaka kuiba kura. Kisiwa hicho kilipiga kura ya mapema jana kwa vikosi vya usalama na makundi mengine maalum ambapo ghasia zilizuka na kusababisha vifo vya watu 10 na wengine kujeruhiwa. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW