1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Kenya zapiga hatua katika kupambana na rushwa-CPI

Daniel Gakuba
31 Januari 2023

Ripoti ya mwaka 2022 ya shirika la kimataifa la kupambana na rushwa, Transparency International inaonyesha kuwa nchi nyingi za Afrika kusini mwa Sahara zimepiga hatua nyuma. Tanzania, Kenya zimepata mafaniko japo madogo.

Transparency International Logo
Picha: Rafael Henrique/ZUMA Wire/IMAGO

Katika ripoti yake, Transparency International inasema 2022 ulikuwa mwaka mwingine wa mkwamo katika ukanda wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, katika vita vya kupambana na rushwa, wastani wa mafanikio ukiwa wa alama 32 kwa 100.

Ripoti hiyo imemulika jinsi rushwa na ufisadi vinavyohujumu juhudi za demokrasia, usalama na maendeleo katika ukanda huo, ambako kati ya nchi 49 zilizochunguzwa, ni tano tu zilizopata juu ya alama 50 kwa 100.

Soma zaidi: Mataifa yanayoongoza kiuchumi yatazamwa kuwa fisadi

Visiwa vya Ushelisheli vimeongoza kwa mara nyingine kwa kupata alama 70 kwa mia, vikifuatiwa na Botswana na Cabo Verde ambazo kila moja imepewa alama 60 kwa 100. Mkiani zipo Burundi na alama 17 na Guinea ya Ikweta iliyopata hizo hizo 17, Sudan Kusini na alama 13 kwa mia, na Somalia ya mwisho kabisa kwa kuambulia lama 12 kwa 100.

Mizozo na ukosefu wa usalama ni vichocheo vya ufisadiPicha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

Kwa Tanzania na Kenya hali inaboreka taratibu

Upande wa Afrika Mashariki Kenya na Tanzania zimeelezwa kufanikiwa kwa kiasi fulani katika mapambano dhidi ya rushwa, zikijiongezea alama sita kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2022. Hata hivyo ikilinganishwa na mwaka jana, Tanzania imepoteza alama moja, huku Kenya ikijiongezea alama mbili.

Rwanda iko katika nafasi ya 54 kimataifa, ikiwa ya tano barani Afrika na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, licha ya kwamba imepoteza alama mbili ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Soma zaidi: Mo Ibrahim: Afrika yapiga hatua katika utawala bora

Transparency International inasema katika faharasa yake ya mwaka 2022 kuwa mizozo ya kidunia kama vita vya Ukraine, mabadiliko ya tabianchi na kupanda kwa gharama ya maisha imekuwa na athari za moja kwa moja kwa ustawi wa ukanda ya Afrika kusini mwa Sahara.

Wahanga wakuu wa rushwa ni wananchi wanyonge wanaokosa huduma za msingiPicha: AP

Mizozo na migogoro ni ''rutuba'' kwa ufisadi

Imeonyesha kuwa nchi kadhaa za ukanda huo zimekabiliwa na mapinduzi ya kijeshi, migogoro ya itikali kali, mashambulizi ya kigaini na ongezeko la visa vya uhalifu, na kuongeza kuwa hali hiyo imedhihirisha kuwa ufisadi hushamiri katika maeneo yenye migogoro.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Sudan Kusini na Somalia zimetolewa mfano kama vielelezo halisi vya uhusiano huo baina ya ufisadi na ukosefu wa usalama.

Soma zaidi: Mizozo yachangia ongezeko la njaa

Aidha, Transparency International imesema kuwa vyombo vya usalama visivyoendeshwa ipasavyo vimeshindwa katika baadhi ya mataifa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mali vimeshindwa kuweka uthabiti ndani ya mataifa husika, na matokeo yake ni kuibuka ututiri wa makundi yenye silaha, ambayo hujihusisha katika shughuli haramu zinazohatarisha usalama wa raia.

Chanzo: Ripoti ya CPI