1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kuendelea na uopoaji katika kivuko cha MV Nyerere

22 Septemba 2018

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuziopoaji maiti na kuwaokoa watu waliozama kwenye kivuko cha MV Nyerere, katika Ziwa Victoria, mpaka pale mwili wa mwisho utakapopatikana.

Tansania Unglück
Picha: DW/S. Khamis

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola amesema baada ya kupatikana kwa mtu mmoja akiwa hai, katika kivuko hicho kilichozama Alhamisi ya tarehe 20.09.2018 wakati kikikaribia kutia nanga katika kisiwa cha Bwisya Ukara, Mwanza, serikali imeona kuna uwezekano wa kuwepo kwa watu wengine walio salama. ''Tukio hili la kupatikana kwa mtu baada ya siku mbili, ni ushahidi tosha kuwa kuna watu wanaweza kuwa wazima ama wamekufa hivyo ni vizuri tukaendelea na zoezi hili la uokoaji na uopoaj'', alisema Waziri Kangi.

Asubuhi ya leo waokoaji na waopoaji wamefanikiwa kumuokoa fundi mkuu wa kivuko hicho, Alphonce Charahani aliyekaa ndani ya maji kwa muda wa zaidi ya saa 48 akiwa hai na kupelekwa katika kituo cha afya cha Bwisya kwa matibabu zaidi. Charahani ameokolewa wakati waokoaji hao wakiwa wanaendelea na zoezi hilo

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali waokoaji leo wamefanikiwa kuiopoa miili mingine 73 na hivyo kuifanya jumla ya miili iliyoopolewa kutoka katika kivuko hicho kufikia zaidi ya 209.

Waokoaji wakiendelea na shughuli za uokoziPicha: DW/S. Khamis

Wakati Charahani akiokolewa kutoka ndani ya kivuko hicho, mwili wake wote ulikuwa umepakwa mafuta ambapo baadhi ya watu wanasema mafuta hayo husaidia maji yasiweze kupita katika vinyweleo.

Tayari zoezi la kuitambua miili ya marehemu limeshaanza ambapo zaidi ya miili 131 imeshatambuliwa mpaka sasa huku serikali ikitoa kiasi cha shilingi laki tano pamoja na jeneza kwa kila mfiwa na tayari baadhi ya marehemu wameshaanza kusafirishwa kwa ajili ya mazishi.

Baadhi ya walionusurika katika ajali hiyo wanasema kivuko hicho kilikuwa kimebeba abiria wengi kupita kiasi pamoja na shehena kubwa ya mizigo kinyume na uwezo wake ambapo kwa mujibu wa Wakala wa Umeme na Ufundi, TEMESA, kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 101 pamoja na tani 25 ya mizigo.

''Wakati tunaanza safari ya kuelekea Bwisya kutoka Bugorola baadhi yetu tuliona jinsi kivuko kilivyozidiwa na hata tulipomwambia nahodha wa kivuko hakujali, wakati tunakaribia kufika Bwisya nilimuona nahodha akiongea na simu na ghafla akaona mwelekeo ukiwa siyo wenyewe na alipojaribu kukirudisha kivuko kwenye mwelekeo wake ndiyo ajali ikatoke baada ya mizigo na magari kuhamia upande mmoj'' alisema mmoja wa abiria aliyekuwemo ndani ya kivuko hicho.

Kivuko cha MV Nyerere kilichozamaPicha: Getty Images/AFP

 

Kivuko cha MV Nyerere kwa muda mrefu kimekuwa kikilalamikiwa kwa ubovu ambapo mwaka huu serikali ilifanya ukarabati wa injini mbili kwa gharama za shilingi milioni 191 baada ya malalamko ya muda mrefu kutoka kwa wenyeji wa kisiwa cha Ukara.

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa ambazo zitafikia ukomo wake siku ya Jumatatu. Mbali na hilo, Rais Magufuli amesema wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote ile kusababisha ajali hiyo wakamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Mpaka sasa kumekuwa na ugumu wa kufahamu takwimu halisi za idadi ya watu waliokuwa wameingia kwenye kivuko hicho baada ya nyaraka zote zinazoonesha kumbukumbu za waliokata tiketi kutokupatiakana.

Mwandishi: Dotto Bulendu
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW