Tanzania yapunguza bei ya mafuta, kupoteza bilioni 100
2 Machi 2022Mamlaka husika nchini Tanzania zinasema hatua ya serikali kuondoa tozo ya shilingi 100 kila mwezi kwa nishati ya mafuta imetokana na sababu mbalimbali zilichochea kupaa kwa bei ya nishati hiyo muhimu katika soko la dunia ikiwemo pia mzozo wa vita vya Ukraine na Urusi.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania, (EWURA) Titus Kaguo amesema serikali ya nchi hiyo imekwishaanza kukabiliana na kitakachotokea siku za usoni.
“Katika setka ya mafuta kwa maana ya petrol, disel na mafuta ya taa, ambayo kiujumla kwa mwezi serikali itapoteza karibu bilioni 30. Sasa unaweza ukaona hiyo ni mipango tayari serikali imeishaanza kukabiliana kile ambacho kinakuja. Serikali bado inachakata ni hatua zipi za kuchukua ili huyu Mtanzania asiumie sana,” alisema Kaguo.
Soma pia: WFP yaonya mzozo wa Ukraine na Urusi huenda ukaathiri bei za bidhaa nchini Yemen
Tangu Urusi iivamie kijeshi Ukraine na kusababisha mzozo wa kivita unaoendelea hivi sasa huku mataifa mbalimbali yakilaani kitendo cha Urusi na kuiwekea vikwazo nchi hiyo, athari zimeanza kuonekana katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Hofu ya mapato zaidi kupotea
“Na huenda miezi ijayo zikaondoka bilioni mia mbili, mia tatu, mia nne na kuendelea kutokana na bei za mafuta zitakavyoongezeka," alisema Dk. Nasibu mramba, mhadhiri wa chuo cha elimu ya biashara CBE, tawi la Dodoma.
"Sasa serikali inabidi kutafuta vyanzo mbadala ili kufidia hilo pengo la bilioni 1oo lazima itafute mahali itakapopata kodi au fedha nyingine ili ziweze kuingizwa pale ambako hiyo bilioni 100 imetolewa lasivyo tutaingia katika nakisi ya bajeti na baadhi ya shughuli za maendeleo hazitatekelezwa," aliongeza.
Soma pia: EU yaonya juu ya umaskini wa mafuta kutokana na mzozo wa nishati
Kupotea kwa kiasi hicho cha mapato ya fedha kila mwezi kunatokana na serikali ya nchi hiyo kuondoa tozo ya shilingi 100 kwa kila lita ya nishati ya petroli, diseli na mafuta ya taa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Hatua ya kuondolewa kwa tozo hiyo ya shilingi 100 katika nishati hiyo imekuja siku za hivi karibuni baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi Oktoba mwaka jana kutoa muongozo uliopunguza baadhi ya tozo katika nishati ya mafuta zenye thamani ya shilingi bilioni 102 ili kupunguza makali ya bei ya nishati hiyo kwa wananchi.