Tanzania kuruhusu uuzaji magogo katika hifadhi ya Selous
14 Mei 2018Tanzania inalenga kuruhusu biashara kubwa ya magogo katika hifadhi ya wanyama pori ya Selous, mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi barani Afrika ambako pia serikali ya Tanzania inapanga kujenga mtambo wa kuzalisha nguvu za umeme unaotumia maji.
Idara ya misitu ya Tanzania TFS inalenga kuuza eneo la miti lenye ukubwa wa karibu mita za mraba milioni 3.5, kulingana na waraka wa zabuni uliotolewa Aprili 25 ambao shirika la habari la Reuters limepata nakala yake. Hifadhi hiyo ya Selous inayotambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (UNESCO) ni nyumbani kwa wanyama wengi maarufu, kama tembo, vifaru weusi, ndege na wanyama wengine.
Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa megawati 2,100 katika maporomoko ya Mto Rufiji ulioko katika hifadhi hiyo unapingwa na wanaharakati wa kutetea mazingira na wanyama.