1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania lawamani kwa kutozuia utumikishwaji wa watoto

18 Novemba 2022

Serikali ya Burundi imeilaumu Tanzania kwa kutozuia usafirishaji na utumikishwaji wa watoto kutoka Burundi wanaoingia Tanzania kwa ajili ya kazi za utumishi majumbani na mashambani.

TABLEAU | Internationaler Tag gegen Kinderarbeit 2021 | Malawi, Lilongwe
Picha: Amos Gumulira/AFP/Getty Images

Manung'uniko hayo juu ya watoto wa Burundi kusafirishwa kutoka Burundi yalianza kuibuka jana katika mkutano wa ujirani mwema uliowahusisha viongozi wa mikoa ya Tanzania na Burundi, ikielezwa kuwa watoto wengi wanapotea.

soma Matatizo ya afya na njaa kwa wanawake yajadiliwa Burundi

Katika mahojiano maalumu na DW mapema leo mkuu wa mkoa wa Makamba nchini Burundi na mwenyekiti wa vikao vya ujirani mwema kati ya Tanzania na Burundi Bi. Francoise Ngozirazana amebainisha kuwa kumekuwepo na wimbi kubwa la watoto wanaotoroka shule nchini Burundi na kuajiriwa mashambani nchini Tanzania. Anatoa wito kwa serikali ya Tanzania kushirikiana na Burundi kuzuia biashara haramu ya usafirishaji wa watoto sambamba na ajira.

soma Wahudumu wa malori wamulikwa juu ya utumikishwaji wa watoto Nakuru

Tanzania yaahidi ushirikiano

Picha: Bujumbura Amida Issa/DW

Tanzania imeahidi kutoa ushirikiano kudhibiti uhamiaji haramu, ajira na usafirishaji wa watoto. Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema taratibu za raia wa nje kuingia nchini kwa ajili ya kufanya shughuli ndogo ndogo za ujasiriamali zinafahamika, hata hivyo watoto hawaruhusiwi kuingizwa kwenye ajira au utumikishwaji mashambani.

Kwa upande wake afisa uhamiaji wa mkoa wa Kigoma anaweka bayana kuwa hakuna anayeruhusiwa kusafirisha wala kuajiri watoto na kwamba wanaokutwa katika ajira mashambani idara ya uhamiaji huwakamata na kuwarejesha nchini mwao huku waliowasafirisha au kuwaajiri wakishtakiwa

Wakulima wengi katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Kagera hutegemea nguvu kazi ya vijana kwa ajili ya shughuli za kilimo jambo linalosababisha kuwepo kwa uhamiaji mwingi usiozingatia sheria.

Kufuatia hali hiyo Burundi imeiomba serikali ya Tanzania kuwafutia mashtaka na kuwarejesha Burundi, wahamiaji wasio na vibali wapatao 5,682 waliokamatwa kwa makosa ya kuingia Tanzania bila vibali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka huu.

 

//Prosper

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW