1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Miaka 25 bila Mwalimu Nyerere

14 Oktoba 2024

Watanzania wamefanya kumbukumbu ya miaka 25 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999. Siku ya Nyerere, inalenga kumuezi mwasisi huyo wa taifa la Tanzania.

Tanzania | Rais wa zamani wa Tanzania Julius Nyerere
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatajwa kuwa kiongozi mwenye maono makubwa.Picha: AFP/Getty Images

Katika maadhimisho haya, wachambuzi wa siasa wamesema kuwa viongozi wa sasa bado hawajaakisi kikamilifu misingi aliyoiweka Nyerere, hasa katika eneo la umoja, maendeleo, na ushirikiano wa kikanda. 

Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya siasa na mwanadiplomasia, ameweka wazi kuwa Nyerere alikuwa na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu, ambayo ni nadra kuona leo.

"Kila mtu anakubali kwamba Mwalimu alijaribu mambo magumu, kiasi ambacho sijui utamtaja nani hivi leo ambaye ameweza kujaribu hata robo ya mambo hayo."

Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere imefanyika kwa namna mbalimbali nchini, ikijumuisha misa maalum na makongamano ya kutafakari urithi wake. Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza maadhimisho hayo akiwa jijini Mwanza, ambapo alihudhuria misa maalum ya kumbukumbu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Fransisko Ksaveri, Nyakahoja. 

Mwalimu Nyerere alikuwa kinara wa diplomasia na harakati za ukombozi Afrika na dunia ya ulimwengu wa tatu.Picha: dpa/picture-alliance

Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere na ushirikiano wa Kiafrika

Akifuatana na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, walitumia muda huo kuzungumzia mazuri aliyoyafanya Nyerere, ikiwa ni pamoja na kuchangia ukombozi wa nchi za Kiafrika. "Chini ya uongozi wake, alitoa rasilimali za nchi kusaidia harakati za ukombozi kwa nchi nyingine," alisema Dk. Mpango.

Naye Kiongozi Mkuu wa chama cha siasa cha ACT Wazalendo, Doroth Semu, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza urithi wa Nyerere kwa vitendo, akilenga mshikamano na amani, vitu ambavyo vilikuwa msingi wa uongozi wake.

Soma pia: Samia: Tumuenzi baba wa taifa kwa kupinga ufisadi

"Alisisitiza kuwa viongozi ni watumishi wa wananchi, wanaopaswa kuwaletea maendeleo na kusimama nao katika kila hatua," alisema kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo.

Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alifariki mwaka 1999, alikuwa si tu mbeba maono wa uhuru wa Tanganyika, bali pia alisaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru. Nchi hizo ni pamoja na Zambia, Malawi, Botswana, Lesotho, Mauritius, Swaziland, na Shelisheli.

Kumbukumbu ya miaka 25 bila Nyerere imewaunganisha Watanzania kutafakari urithi wake, huku wakihamasishwa kuendeleza msingi wa uongozi bora aliouacha kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Bibi Titi Mohamed: "Mama wa Taifa" Tanzania

02:03

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW