1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: miaka 30 jela kwa Mkuu wazamani wa Wilaya ya Hai

Veronica Natalis15 Oktoba 2021

Mahakama ya hakimu Mkazi iliyopo Arusha, imemuhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Tansania | East African Court of Justice in Arusha
Picha: DW/V. Natzalis

Hii ni kesi ya kwanza kwa kiongozi wa umma nchini Tanzania kuhukumiwa  tangu Rais Samia Suluhu Hassani aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu. 

Akisoma hukumu hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya Arusha Odira Amworo amesema kuwa ameridhika na mashitaka dhidi ya Sabaya na wenzake na kwamba  kati ya mashahidi 11 waliotoa Ushahidi wao dhidi ya Sabaya ni mashahidi wawili tu ambao Ushahidi wao haukuwa na mashiko.

Soma pia:Jaji Luvanda ajitoa katika kesi ya CHADEMA 

Mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha

Lengai Ole Sabaya mwenye umri wa miaka 35  aliyeapishwa kuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro mwezi Julai mwaka 2018, anakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha, huku miongoni mwa mashitaka hayo  wizi wa shilingi milioni 769 mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad, wizi uliofanyika jijini Arusha.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa kabla na baada ya kufanya tukio hilo washitakiwa waliwashambulia watu watano kwa kuwapiga na bunduki ili kufanikisha wizi huo. 

Katika shitaka la pili, Sabaya na wenzake wawili waliiba shilingi laki tatu na elfu 90 kutoka kwa diwani wa kata ya Sombetini Bakari Msangi, wakiwa katika mtaa wa bondeni jiji Arusha.

Soma pia: CPJ yaitaka Tanzania kumuachia huru mchora katuni John Fwema

Sabaya ajitetea kabla ya hukumu

Kabla yakusomwa kwa hukumu Sabaya alitakiwa kujitetea akaiomba mahakama imuonee huruma kwani hayakuwa maamuzi yake bali alikuwa anatekeleza maagizo ya mamlaka zake za uteuzi na pia anamchumba aliyemtolea mahari na wanatarajia kufunga ndoa. 

Kabla ya kuanza kusomwa kwa hukumu hiyo wakili wa Serikali Felix Kwetukia alisema upande wa Jamhuri upo tayari kusikiliza hukumu hiyo iliyofuatiliwa na wengi.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza juni 4 mwaka huu, baada ya kukamatwa siku ya tarehe 27 mwezi May wilaya ya Kinondoni Jijini Dare Es Salaam. Katika mahakama hii ulinzi uliimarishwa huku kukiwa na watu wengi waliosubiri kujua hatma ya kesi hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW