1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Msumbiji kushirikiana kupiga vita ugaidi

Daniel Gakuba
22 Septemba 2022

Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kushirikiana katika kupiga vita ugaidi na uhalifu kwenye mpaka wao wa pamoja. Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini Msumbiji.

Mosambik Militär SADC SANDF
Msumbiji imekabiliwa na vurugu za uasi kwa miaka mitano iliyopitaPicha: Alfredo Zuniga/AFP/Getty Images

Taarifa rasmi za serikali ya Msumbiji zimeeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewitembelea nchi hiyo jirani kwa mualiko wa serikali ya Maputo, nia ikiwa ni kuimarisha uhusiano wa kirafiki na kidugu baina ya nchi hizo.

Uhusiano huo mwema umetiliwa mkazo na Rais Samia, ambaye katika hotuba yake amesema Tanzania na Msumbiji zimekuwa na maoni sawa tangu kupigania ukombozi wa Mwafrika, hadi mapambano kwa ajili ya usawa na kujitegemea kiuchumi.

Soma zaidi: Tanzania na Msumbiji wajadili kupambana na uasi

Tangazo la Ikulu ya Tanzania limesema waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Stergomena  Tax na mwenzake wa Msumbiji Cristovao  Chume wamesaini mkataba wa ushirikiano katika nyanja za amani na usalama.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu HassanPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Rais Samia asifu ushirikiano wa kihistoria

Mkataba huo umekuwa nambari moja kwenye orodha ya masuala yaliyotajwa na Rais Samia miongoni mwa yaliyofikiwa katika mazungumzo baina yake na rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi.

''Kama mnavyojua nyote, Tanzania na Msumbiji zina mtazamo sawa kuhusiana na amani na usalama wa kikanda, kati ya nchi na nchi, na kwa ngazi ya dunia, '' amesema Rais Samia Suluhu Hassan na kuongeza kuwa  tangu miaka ya 1960 Tanzania na Msumbiji zimekuwa na ushirikiano katika sekta za ulinzi na usalama.

''Katika mazungumzo yetu tumeafikiana kuendeleza ushirika huo katika kupiga vita ugaidi, vitendo vya vurugu, na uhalifu mwingine wa kuvuka mipaka,'' amesema.

Soma zaidi: Wakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji 

Kwa takribani miaka mitano iliyopita, Msumbiji imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya waasi ambayo yameuwa maelfu ya watu na kuwalazimisha maelfu wengine kuyahama makaazi yao.

Filipe Nyusi, rais wa MsumbijiPicha: DW

Mnamo miezi ya hivi karibuni maisha yameanza kurejea baada ya waasi hao kufurushwa kwa msaada wa vikosi vya nchi za Kiafrika.

Nyusi asema ushirikiano wa kikanda umekuwa wenye tija

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema nchi yake na Tanzania tayari zimekuwa zikishirikiana katika hilo.

''Kwa nyakati tofauti tulipoizuru Tanzania, tulilizungumzia suala hili, na juhudi za pamoja za kiusalama tayari zinafanyika. Juhudi hizo zimesaidia dkuvidhibiti vitendo vya adui, hata kabla ya kuanzishwa kwa ujumbe wa SAMIM,'' amesema Rais Nyusi.

SAMIM ni ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC, kwa ajili ya kupambana na ugaidi nchini Msumbiji.

Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyokubaliwa wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Msumbiji ni kilimo, uvuvi na uchimbaji wa mafuta na gesi, pamoja na programu ya miaka mitano ya kubadilishana wanafunzi. Rais Samia pia ameahidi kuwapeleka wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini Msumbiji, kusaidia ufundishaji wa lugha hiyo kuanzia ngazi ya shule za msingi.

-afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW