1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: mtoto mwenye ualbino atoweka

Goorge Njogopa6 Juni 2024

Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema bado linaendelea na msako wa watuhumiwa wa kupotea kwa mtoto mmoja mwenye ulemavu wa ngozi - albino.

Watoto wenye ulemavu wa ngozi Tanzania
Polisi inasema tayari limewatia mbaroni watuhumiwa watatu, na haiwezi kusema lolote kuhusu hatma ya uchunguzi wakePicha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Watetezi wa haki za binadamu wanatoa mwito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za haraka kukabiliana na wimbi hilo linaloanza kujitokeza katika wakati huu msimu wa uchaguzi ukikaribia. 

Wakati jeshi hilo likisema tayari limewatia mbaroni watuhumiwa watatu, na kusisitiza kwamba bado haliwezi kusema lolote kuhusu hatma ya uchunguzi wake, watetezi wa haki za binadamu wanasema wanaona wimbi jipya la kuandamwa watu wenye ualbino linaanza kichipuka upya hasa wakati huu wa kuelekea katika chaguzi za usoni.

Mtoto huyo mwenye ualbino, Asiimwe Novath, aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu alichukuliwa nyumbani kwao kaskazini magharibi mwa nchi katika kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita..

Unyanyapaa dhidi ya walemavu wa ngozi ungalipo

01:21

This browser does not support the video element.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Blacius Chatanda aliyezungumza na DW, mbali ya kuwatia mbaroni watuhumiwa watatu, bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na kwamba pia hatma ya mtoto huyo bado haijulikani.

Wakati jeshi la polisi likichukua hatua hizo za uchunguzi, makundi ya utetezi wa haki za binadamu yanasema kujirudia tena vitendo vya kuwaandama watu wenye ualibino ni kasumba mbaya na kuwatia hofu watu wa jamii hiyo.

Kwa takribani miaka kumi sasa, matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino yalipungua kwa kiasi kikubwa, lakini sasa tukio la kutekwa kwa mtoto huyo kumeishitua jamii na kuanzisha hofu mpya.

Akizungumzia tukio hilo, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, wakili Maduhu William, mbali ya kumsihi Rais Samia kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo, lakini pia amefungamanisha matukio ya namna hiyo na mazingira ya uchaguzi.

Matukio ya kuwawinda watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania yanahusishwa na imani potofu za kishirikinaPicha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Hata hivyo, jeshi la polisi linasema haliwezi kubainisha moja kwa moja kuwa hayo yanayotokea yanafungamanishwa na mazingira ya uchaguzi au ni vitendo vya ushirikina tu:

Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania, Godson  Mollel, anasema kuanza kujiri tena kwa matukio ya namna hiyo ya kikatili ni jambo la kuchukiza sana mbele ya uso wa binadamu, wapenda haki na kwa namna nyingine kunaashiria namna wimbi la vitendo vya kishirikina linavyoendelea kuzunguka ndani ya jamii:

Matukio hayo yaliyolikumba eneo la kanda ya Ziwa Viktoria yalivuma zaidi katika kipindi cha miaka kumi kurudi nyuma, lakini kutokana na kampeni kubwa iliyochukuliwa wakati huo vitendo hivyo vilizimika.

Hata hivyo, kuanza kuchomoza tena kwa matukio hayo ya kikatili kunatuma ujumbe mwingine kwa mamlaka kuhusu ulazima wa hatua za haraka.