1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania na Kenya zadaiwa kuwakandamiza raia wake

20 Aprili 2026

Kenya na Tanzania zimeingia kwenye orodha ya nchi zinazotuhumiwa kufanya ukandamizaji wa raia wao nje ya mipaka, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la haki za binadamu la Freedom House.

Picha ya Pamoja | Samia Suluhu Hassan na William Ruto
Picha ya Pamoja ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Kenya William RutoPicha: Ericky Boniphace/Urs Flueeler/AFP

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka 2025 ulishuhudia ongezeko la vitendo vya kile kinachoitwa "ukandamizaji wa kuvuka mipaka,” ambapo serikali huwafuatilia, kuwakamata au hata kuwarejesha kwa nguvu wakosoaji wao walioko nje ya nchi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, China inaongoza duniani kwa vitendo hivyo, ikifuatiwa na Vietnam na Urusi, huku Kenya na Tanzania zikiorodheshwa kwa mara ya kwanza pamoja na nchi nyingine kadhaa zikiwemo Afghanistan na Zimbabwe. Kwa ujumla, takribani nchi 54 duniani sasa zinahusishwa na vitendo hivyo tangu mwaka 2014, sawa na zaidi ya robo ya mataifa yote duniani.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Afrika Mashariki imeibuka kama moja ya maeneo yanayoongoza kwa matukio hayo, ambapo zaidi ya nusu ya visa vilivyoripotiwa mwaka uliopita vilitokea katika ukanda huo pamoja na Asia ya Kusini Mashariki.

Mwandishi mwenza wa ripoti hiyo, Yana Gorokhovskaia, anaeleza kuwa kuna ushirikiano unaokua kati ya baadhi ya serikali katika ukanda huu, zikiwemo Kenya, Uganda na Tanzania, katika kuwafuatilia na hata kubadilishana wakosoaji ili waweze kukamatwa.

Mifano iliyotolewa ni pamoja na tukio la mwaka 2024 ambapo kiongozi wa upinzani wa Uganda, alitekwa akiwa Kenya na kupelekwa Uganda, anakokabiliwa na mashtaka ya uhaini.Picha: BADRU KATUMBA/AFP

Mifano iliyotolewa ni pamoja na tukio la mwaka 2024 ambapo kiongozi wa upinzani wa Uganda, alitekwa akiwa Kenya na kupelekwa Uganda, anakokabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Pia Januari mwaka 2025, mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Tanzania, Maria Sarungi Tsehai,alitekwa jijini Nairobi kabla ya kuachiliwa kufuatia shinikizo la wanaharakati na vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbinu zinazotumika zaidi ni kukamatwa kiholela na kurejeshwa kwa nguvu kwa wakosoaji, hali inayochochewa na kile kinachoelezwa kuwa ni shinikizo la kisiasa, hususan wakati wa chaguzi.

Shirika la Freedom House linaonya kuwa mwenendo huu ni njia rahisi na ya gharama ndogo kwa tawala kudhibiti upinzani, huku likizitaka nchi zenye mifumo ya kidemokrasia kuchukua hatua kali, ikiwemo vikwazo dhidi ya viongozi wanaohusika na vitendo hivyo.

Hata hivyo, wachambuzi wanaeleza kuwa licha ya ukosoaji wa kimataifa, mara nyingi shinikizo hilo hudumu kwa muda mfupi kabla ya mahusiano ya kidiplomasia kurejea katika hali ya kawaida.

Kuingia kwa Kenya na Tanzania katika orodha hiyo kunaibua maswali mapya kuhusu mwelekeo wa haki za binadamu katika kanda ya Afrika Mashariki na mustakabali wa usalama wa wakosoaji wa serikali ndani na nje ya mipaka yao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW