1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Serikali zingatieni utaalamu kwenye chanjo

Admin.WagnerD29 Januari 2021

Chama cha Wananchi CUF kimeitaka serikali ya Tanzania kuwahusisha wataalamu katika kutathmini chanjo yenye ubora inayoweza kutumika nchini humo dhidi ya virusi vya corona.

Afrika Tansania Mosambik SADC  John Magufuli
Picha: DW/D. Khamis

Chama cha Wananchi CUF kimeitaka serikali ya Tanzania kukusanya jopo la wataalamu na kutathmini ubora wa chanjo inayoweza kutumika nchini humo dhidi ya virusi vya corona, badala ya kuzikataa bila ya kuweka hadharani sababu ya kuzipinga.

Chama hicho cha upinzan kinatoa tamko hilo ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli kuweka hadharani msimamo wa serikali yake kutounga mkono utumiaji wa chanjo hiyo ambayo tayari baadhi ya mataifa ulimwenguni wameipokea kama tumaini jipya dhidi ya virusi vya corona.

Mapema leo chama hicho kimewaambia waandishi wa habari kuwa, kinaunga mkono maamuzi ya Rais Magufuli ya kutoliwekea taifa vizuizi ili kupambana na janga la COVID-19, lakini kuna haja serikali kujitatmini upya juu ya chanjo ya aina gani taifa itatumia ili kukabiliana na janga hilo ambalo limewahi kuwaathiri watu kadhaa hapa nchini kabla ya serikali kutangaza kuwa huru dhidi ya virusi vya corona.

Rais John Magufuli wa Tanzania anatilia shaka chanjo zinazotoka mataifa ya kigeniPicha: Martin Wagner/imago images

Mohammed Ngulangwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho anasema, serikali iteue jopo la wataalamu na litathnini aina gani ya chanjo italifaa taifa na iweke utaratibu mwepesi usio wa ghali wa kupima maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha, chama hicho cha CUF kimeitaka serikali kuwa na ushirikianao wa karibu na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la virusi vya corona, kwani taifa hilo sio kisiwa na tayari imeridhia mikataba kadhaa ya kushirikiana katika wakati mgumu kama huu ambao dunia inapitia.

Tamko hili linaungwa mkono na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC wao wakiitaka serikali iifanyie utafiti chanjo hiyo iliothibithishwa na WHO na kama wakiona haitafaa kwa matumizi hapa nchini basi itoke na sababu hadharani. Anna Henga ni mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho.

Baadhi ya wananchi na wadau wa masuala ya afya wameiambia DW kuwa, wanaunga mkono kauli ya Rais Magufuli ya kutoipitisha chanjo hiyo ya virusi vya corona. 

Mwandishi: Hawa Bihoga