1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Ushahidi mpya juu ya mauaji ya Oktoba 2025

21 Januari 2026

Machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 2025 nchini Tanzania yalifunikwa na giza zito la kuzimwa kwa intaneti, baada ya mrindimo wa bunduki kunyamaza ghafla.

Polisi karibu na bango la uchaguzi la Samia Suluhu Hassan lililoharibiwa - 30.10.2025
Polisi karibu na bango la uchaguzi la Rais Samia Suluhu Hassan lililoharibiwa - 30.10.2025Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Sasa, ushahidi mpya unafichua kile ambacho hakikusimuliwa – vifo vya watu ambao idadi yao bado haijulikani, miili iliyotoweka, na tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama. 

Ingawa yaliyotokea katika jiji la pili kwa ukubwa nchini Tanzania, Mwanza, wakati wa machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 2025 hayajafahamika kwa undani, ushahidi wa walioathirika unaonyesha mauaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama, ambao uliwalenga hata watu ambao hawakuhusika na maandamano.

Hadithi, uvumi na simulizi za mashahidi wa mauaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba nchini Tanzani ziko kila mahali. Hadi sasa idadi halisi ya vifo haijulikani, lakini makadirio ya Umoja wa Mataifa yanaonyesha "angalau watu 700" walipoteza maisha katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wazeePicha: State House

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassanalisema serikali yake ilikuwa ikipambana na waporaji na watu waliotaka kupindua serikali. ''Tunaposhutumiwa kwa kutumia nguvu nyingi kwenye tukio lile, walitaka tutumie kiwango gani cha nguvu hata iwe kidogo?'' aliuliza Rais Samia katika mkutano na wazee wa Dar es Salaam, na kuongeza, ''Je, tulipaswa kukaa na kuwatazama waandamanaji waliotaka kufanya mapinduzi hadi wafanikiwe?''

Mwangaza juu ya Mwanza


Uchunguzi wa DW umegundua matukio mawili jijini Mwanza ambayo yanapingana na kauli hii. Umebaini kwamba polisi walitumia nguvu kupita kiasi si tu dhidi ya waandamanaji bali pia dhidi ya raia ambao hata hawakuwa wakiandamana. Vikosi vya usalama viliwashambulia na kuwaua watu wasiokuwa na silaha.

Kituo cha kupigia kura chateketezwa moto wakati wa maandamano wakati wa uchaguzi wa raisPicha: AFP

Maandamano ya siku ya uchaguzi yalianzia Dar es Salaam na baadaye yakaenea hadi miji mingine kama vile Arusha, Dodoma na Mwanza. Wakati huo, kulikuwa na Watanzania waliokuwa hawaridhiki na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, kukandamizwa kwa upinzani na matendo ya kikatili dhidi ya raia.

Vikosi vya usalama vilionekana mahala kadhaa na vurugu zilianza kwa haraka    katika maandamano ya mitaani na maeneo mengine kote nchini. Mabasi na vituo vya mafuta vilichomwa moto, na kiwanda cha magodoro kilivamiwa na kuporwa.

Giza totoro la mawasiliano baada ya kukatwa kwa intaneti

Serikali ilitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni na kuzima mtandao wa intaneti, hatua iliyoitenga Tanzania na ulimwengu wote.

Lakini hilo lilichelewesha tu kuenea kwa taarifa. Katika wiki zilizofuata baada ya uchaguzi, DW iliweza kufuatilia ushahidi kuhusu matukio mawili mahususi ya vurugu huko Mwanza, jiji la pili kwa ukubwa nchini Tanzania. Mashahidi na manusura wameeleza kwamba polisi waliwaua watu wengi kwa risasi katika maandamano na wengine katika nyumba zao.

Waandamanaji mbele ya majengo yanayochomwa moto wakati wa maandamano ya uchaguziPicha: AFP

Serikali ya Tanzania bado inaendelea kuchunguza. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kwamba angalau watu 700 waliuawa, huku upinzani ukisema idadi hiyo ni karibu 2,000.
DW haiwezi kuthibitisha idadi kamili ya vifo lakini inaweza kuthibitisha kwamba polisi waliwafuata na kuwaua raia ambao hawakuhusika katika maandamano. Hilo linapingana na kauli ya Rais Suluhu Hassan kwamba walioandamwa waliazimia kuipindua serikali.

Undani matukio haya mawili makubwa jijini Mwanza

Manusura na mashuhuda walikubali tu kuzungumza na DW kwa sharti la kutotajwa majina. Wanasema kwamba polisi wanajaribu kuwanyamazisha na kuharibu ushahidi. Kwa hivyo, tumebadilisha majina yao kwa usalama wao.

Uchunguzi wetu umegundua kwamba polisi waliwaua watu wanne katika tukio moja huko Kisesa yapata saa moja usiku wa Oktoba 29. Vikosi vya usalama vilijazana eneo hilo kufuatia maandamano ya siku hiyo. Barabara kati ya Kisesa na Mji Mwema  kitongoji cha Mwanza kilicho umbali wa kilomita 14 hivi ilikuwa njia ya kifo mnamo Oktoba 29 hadi 30.

Mauaji ya Kisesa na shida ya kukusanya maiti


Shahidi ambaye tumempa jina la Nuru, akisimulia mauaji ya mmoja wa wahanga, Akida, anasema alikuwa ameketi nyuma ya nyumba yake na vijana wengine wawili.

 ''Walikuwa wakila chipsi. Kisha polisi walifika na kuwaambia wajipange. Kuna saluni karibu, na kulikuwa na kijana anayemaliza zamu yake hapo. Polisi walimwambia ajiunge na wengine ambao tayari walikuwa wamejipanga.''

Maandamano siku ya uchaguzi wakati wa uchaguzi wa rais na wabungePicha: AP Photo/dpa/picture alliance

Anaendelea kueleza kuwa polisi waliwaamuru walale. Walilala. Yule kijana kutoka saluni alijaribu kukimbia, na polisi walimpiga risasi mgongoni. ''Walimpiga risasi tena kifuani kisha wakampiga risasi kichwani. Wale waliokuwa wameamriwa walale chini nao wote walipigwa risasi na kufa.''

Wahanga wa mauaji haya walikuwa Akida, mwenye umri wa miaka 31, Chacha — mwanamme kutoka saluni, mwenye umri wa miaka 40, Hamu, mwenye umri wa miaka 31, na Zuberi mwenye umri wa miaka 24. Mama yake Akida na wengine wawili walishuhudia mauaji hayo ya halaiki.

Ushahidi mwingine ni wa mama mzazi wa mwathirika, ''Nilikimbilia barabarani na kukuta miili minne ikiwa imelala chini. Nilimwinua mwanangu; mwili wake ulikuwa baridi, lakini miguu yake ilikuwa bado na joto kidogo kwa hivyo, nilidhani bado yuko hai. Nilikimbia kurudi nyumbani kuchukua gari. Nilirudi haraka kwenye eneo la tukio. Lakini niligundua kuwa mwanangu alikuwa tayari amekufa.''

Mashahidi wanasema ufyatuaji risasi wa hapa na pale usiku kucha ulifanya iwe vigumu kwa familia za waathiriwa kukusanya miili ya marehemu.

Tanga (sio jina lake halisi) shahidi wa mauaji ya Kisesa anasema kulikuwa na miili mingi mitaani, na hakukuwa na mtu wa kuikusanya.

''Hata kama angekuwa rafiki yako, baada ya kupigwa risasi, ungeweza kukimbia tu - usingethubutu kurudi kuuchukua mwili wake. Hatukuweza hata kuiweka miili kando. Kwa hivyo, kuhusu miili, wanajeshi walikuwa wakiikusanya. Walikuwa na malori maalum kwa ajili ya kubeba miili.''

Mauti kwenye banda la video Tukio la pili jijini Mwanza linaonyesha kwamba vikosi vya usalama havikuwapiga risasi watu wa kawaida mitaani tu. DW iligundua kuwa watu kadhaa walipigwa risasi kwenye ukumbi wa video, maarufu kama Kibandaumiza, huko Mji Mwema kati ya saa moja na mbili usiku mnamo Oktoba 30. Imani - aliyenusurika  alikuwa ameketi hapo na wenzake 14 waliposikia ufyatuaji risasi wa hapa na pale nje. Imani anasema walikuwa ndani wakiangalia taarifa ya habari, mara ghafla, walisikia risasi zikifyatuliwa nje. ''Baadhi yetu tulikuwa tumejificha chini ya benchi. Tulipolala chini, nilisikia risasi zikifyatuliwa tena. Nilihisi kama zilikuwa zikifyatuliwa hewani, lakini kwa kweli zilikuwa zikitupiga sisi.''

Anasema tukio zima lilichukua chini ya dakika moja, kisha wafyatuaji wakaondoka. ''Nilihisi umotoumoto kwenye shavu langu na nilipojigusa kwa vidole vyangu, nilihisi nilikuwa nikigusa meno yangu. Nyama ya shavu langu ilikuwa imekatika. Nilikuwa nimepigwa risasi.''

''Niliona watu wakigaragara tu, na damu zilikuwa zikiwatoka. Nilisimama na kukimbia. Nilijificha kwa muda mahali kisha nikarudi nyumbani,'' alisimulia Imani ambaye jina lake halisi limehifadhiwa. Imani alihangaikia matibabu hospitalini. Na hadi sasa ana wasiwasi kuhusu usalama wake. Hii ndiyo hali baada ya tukio hilo.

Mashahidi wanasema miili kadhaa ililala ndani na karibu na ukumbi wa video, ama Kibandaumiza, hiki. Neema aliwapoteza watu wake wawili katika tukio hili, mwanawe; Simba na mdogo wake, Khamisi. 'Nilitoka kwenda kumsaidia mtu ambaye alikuwa amepigwa risasi mgongoni na pajani; alifanikiwa kujikokota hadi mlangoni mwetu. Alipona. Tulipokuwa tukimsaidia, kijana mmoja alikuja akipiga makelele, "Mama Simba, njoo uone  Mjomba Khamisi na Jabali wameuawa!"

Neema alisema alipiga makelele na kujaribu kuvuuka barabara akiwa na kundi la watu, akiwemo kaka yake Jabali, lakini risasi ziliendelea kurindima. ''Ilibidi turudi. Kisha kijana mwingine akafika na kuniambia, Simba ameuawa.''

Kaka, hawa watu watatuua, tukimbie.


Usi - manusura mwingine wa mauaji ya Mji mwema - alikuwa na Simba ufyatuaji risasi ulipoanza.''Nilimwambia Simba, tunahitaji kukimbia lakini alikataa. Alisema, Hatujafanya kosa lolote; tutulie tu.' Ingawa moyo wangu uliniambia vinginevyo, nilikaa kwa muda. Kisha risasi zaidi zilifyatuliwa.''

 ''Nilimsihi tena: 'Kaka, hawa watu watatuua. Tukimbie.' Lakini aling'ang'ania kama kwamba roho yake ilikuwa ikimwambia abaki hapo. Niligundua njia pekee ya kuokoka ilikuwa kukimbia moja kwa moja kupitia walipo wale maafisa.''

''Nikachomoka. Nilidhani Simba alikuwa nyuma yangu, lakini nilipofika nyumbani kwa mama yake na kugeuka, hakuwepo. Nilitaka kurudi kwenye eneo la tukio, lakini nilisikia mripuko mkubwa - kama bomu. Dakika chache baadaye, simu yangu ilianza kuita ikisema marafiki zetu wameuawa huko Mji Mwema. Simba alikuwa mmoja wao.''

Kulingana na simulizi za mashahidi na data za eneo la kijiografia zilizokusanywa na DW, wauaji walikifikia kibanda cha video wakitokea upande wa kusini. Kwanza waliwashambulia watu karibu na Kanisa la TAG Nyasaka. Kisha wakaenda umbali wa dakika moja hadi kwenye jengo lenye umbo la ''L'' ambalo lilikuwa karibu na kibanda hicho cha video, ama Kibandaumiza.

AK-47 ilitumika kuwaua raia

DW imepata risasi kadhaa kutoka kwenye matukio hayo mawili. Kulingana na mtaalamu wa silaha, Byron Adera, risasi kama hizo kwa kawaida hutumika na bunduki za AK-47.

Byron Adera, mtaalamu wa balistiki anasema kwa kuzingatia muundo wa risasi zilizo mikononi mwa watu mbalimbali zinaendana na kile, unachoweza kusema ni, 7.62, kwa 39mm.
''Ni risasi zinazotumiwa sana na silaha ndogo ndogo na nyepesi za asili, tuseme, aina za AK-47. Nchini Tanzania, silaha ndogo na nyepesi za aina ya AK-47 ambazo hutokea kwenye safu ya kwanza, mifumo mingi ya silaha za mstari wa kwanza ziko mikononi mwa polisi wa Tanzania. Na, bila shaka, vikosi vya ulinzi, vinatumia silaha aina za AK-47.''

Askofu Mkuu Ruwa'ichi aongoza ibada ya ukumbusho kwa waathiriwa wa maandamano ya uchaguziPicha: Ericky Boniphace/DW

Lakini suali ni kwamba je, wauaji walikuwa akina nani? Huko Kisesa, mashahidi wanasema walikuwa polisi wa kawaida wakiwa wamevalia sare. Huko Mji Mwema, wauaji wanatajwa kuwa watu waliovalia mavazi meusi na wengine nguo za kawaida za kiraia. Lakini wote walikuwa na silaha.

Pia DW imegundua kwamba baada ya mauaji huko Kisesa na Mji Mwema, wanajeshi walifika kukusanya miili hiyo na kuipeleka katika Hospitali ya Sekou Toure na Kituo cha Matibabu cha Bugando. Mama yake Akida alienda Bugando kuusaka mwili wake siku moja tu baada ya kuuawa kwake, lakini hawakuupata mwili hadi siku kadhaa baadaye:

'''Kulikuwa na miili mingi iliyorundikana kila mahali,'' anasema Mama Akida,   na kuongeza kuwa walifanikiwa kumpata kando na kutakiwa walipe shilingi 300,000. Hiyo ilikuwa Jumamosi Novemba 1 walipouona mwili kwa mara ya kwanza.

''Siku hiyo ilipita, Jumapili, Jumatatu, na Jumanne. Ilikuwa Jumatano wakati mdogo wangu alipopokea simu kutoka kwa Afisa wa Polisi wa Wilaya ambaye alimwambia kwamba sasa tunaweza kuuchukua mwili kwa mazishi. Tuliuchukua mwili kwa ibada fupi nyumbani na nyingine kanisani na tukaenda Bujore kumzika.''

Bado yanasalia maswali magumu yasio na majibu


Kulingana na ripoti ya ndani ya polisi mkoani Mwanza ambayo ilivujishwa kwa DW, kulikuwa na "raia 68 waliopoteza maisha." Polisi waliwatambua watu 58 kwa majina; baadhi yao walipigwa risasi katika matukio tuliyoyachunguza. Ripoti hiyo haitaji chochote kuhusu matumizi mabaya ya nguvu za jeshi la polisi lakini inadai kwamba kulikuwa na matukio ya vurugu na ghasia.

DW iliwapigia simu polisi wa Mwanza mara kadhaa na kuiomba serikali ya Tanzania kutoa tamko lao kuhusu matukio hayo mawili jijini Mwanza. Tulimwandikia msemaji wa serikali, lakini hakukuwa na majibu.

Je, bado unakumbuka kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan?


Uchunguzi wa DW umegundua kuwa nguvu kupita kiasi ilitumika dhidi ya raia wasio na hatia na kwamba serikali inaweza kuwa na masuali mengi zaidi ya kujibu.

Mamia ya watu bado hawajulikani walipo baada ya ukandamizaji mkali wa wakati wa uchaguzi wa Oktoba 2025.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW