1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Wafanyabiashara walilia hali ngumu ya uchumi

George Njogopa23 Desemba 2020

Kumekuwa na kilio kikubwa kwa jamii ya wafanyabiashara nchini Tanzania wakati huu wa kuelekea msimu wa sikukuu ya Krismasi ambako wanadai hali ya biashara imedorora tofauti na miaka ya nyuma katika msimu kama huu.

Tansania Dar Es Salaam | Kariakoo Markt | Händler
Picha: Said Khamis/DW

Msimu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya mara nyingi huwa ni wa mavuno kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na wale wakubwa, lakini safari hii hali imebadilika na badala yake ni kilio na masikitiko yakitawala miongoni mwao,

Wafanyabiashara wa maduka ya nguo, mapambo pamoja na vyakula wote wanaonekana kukumbwa na hali hii wakisema mauzo yao kwa siku wanayafanya kwa kubahatisha tu.

Wengi wao wanaonyesha wasiwasi wa kuporomoka kibiashara hasa kutokana na hali ya soko inavyozidi kuwa ngumu.

Mkaazi wa Dar es Salaam akichagua nguo kwa ajili ya mwanae katika mtaa wa Kongo sokoni Kariakoo Dar Es Salaam.Picha: Said Khamis/DW

Je, vyuma 'vimebana zaidi'?

Haijafahamika mara moja sababu za kushuka kwa kiasi kukubwa hivi wakati huu wa sikukuu na wengine wakidhani ule usemi wa vyuma kubana pengine ikawa sababu mojawapo.

Lakini, baadhi ya wafanyabiashara wenyewe wanasema kuanguka kwa mauzo kunatokana na sababu nyingine ikiwamo pia ushindani wa kibiashara unaoendelea kujitojeza kama vile kushamiri kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wanaofahamika kama wamachinga.

Wafanya biashara wasema wanunuzi wamekuwa adimu mno msimu huu wa Krismasi 2020.Picha: Said Khamis/DW

Wasiwasi unazidi kuwakabili wafanyabiashara hao hasa wakitambua kuwa mwezi Januari ndiyo unakaribia ambao unaambatana na majukumu mengine kama vile ada za shule za watoto pamoja na urejeshaji wa mikopo kwa wale waliopata mitaji kwa njia ya mikopo.

Faida tele kwa wauzaji wa vileo

Kwa upande mwingine wa shilingi ni neema kwa wauzaji wa vileo kama vile bia na pombe kali na baa nyingi ikiwamo pia sehemu za starehe mauzo bado yako juu. Watu wanaendelea kuserebuka wakijipongeza kwa kukaribia kuumaliza mwaka na kusherehekea sikukuu ya Krismasi.

Wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi ya mikoani nako pia harufu ya neema inashuhudiwa na inaelezwa kwamba kumekuwa na shida kubwa ya kupata tiketi ya kusafiri wakati huu kutokana na mahitaji makubwa yanayoendelea kushuhudiwa.

Usiidharau shilingi

06:12

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW