1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaanza zoezi maalum la kuhesabu watu na makaazi

23 Agosti 2022

Tanzania inafanya zoezi lasensa ya watu na makaazi itakayoendelea kwa muda siku saba, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa miongoni mwa viongozi waliokwishahesabiwa mapema kabisa.

EAC Staaten Video-Konferenz | Samia Suluhu Hassan
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Rais Samia amewatolea mwito wananchi kuendelea kutoa ushirikiano zaidi wakati wa zoezi hilo akisisitiza kuwa sensa ni kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Amesema sensa ya safari hii inafanywa kitaalamu zaidi ikitumia teknolojia mamboleo na kwamba taarifa zitakazokusanywa zitatumika kama  mwongozo kwa serikali kupanga na kuratibu shughuli za kimaendeleo.

"Niwaombe tu wananchi wakae na taarifa zao tayari ili makarani waweze kufanya kazi zao haraka haraka, baada ya kusema hayo, tuitakie nchi yetu zoezi jema, tuwatakie makarani wafanye kazi zao kwa ufanisi, na wanachi wajitokeze kutoa majawabu ambayo yanatakiwa," alisema Rais Samia Suluhu Hassan.  

Makamu wa rais Tanzania Dkt Philip MpangoPicha: DW/S. Khamis

Makamu wa rais ahimiza raia wa tanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la sensa

Wakati Rais Samia akiwa amehesabiwa Ikulu Chimwino jijini Dodoma, Makamu wa Rais Dr Philip Mpangio amehesabiwa jijini Dar es salaam na ametumua nafasi hiyo kuwarai wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo.

"Ndio maana nimekaa hapa nimetulia na familia yangu, nimehesabiwa vizuri, kuanzia mimi, mke wangu, watoto waliolala hapa nyumbani, vijana wangu wategemezi ninaokaa nao humu ndani, wajukuu nilio nao humu nao zote taarifa nimezotoa kwahiyo nawaomba na wengine wafanye hivyo hivyo," alisema Makamu wa Rais Dkt Philip Mpangio.

Naye waziri mkuu Kassim Majaliwa amekshiriki zoezi hilo kwa kuhesabiwa jimboni kwake Ruangwa mkoani Lindi, wakati viongozi wengine wa kisiasa na kidini wakijitokeza katika maeneo mbalimbali.

Kulingana na Kamisaa mkuu wa sensa, Anne Makinda, sensa hii ya watu na makazi inatarajiwa kudumu kwa muda wa siku saba. Ili kufanikisha katika siku yake ya kwanza, serikali iliitangaza siku ya leo kuwa siku ya mapumiziko ya taifa ili kutofa fursa kwa wanachi kushiriki kikamilifu.

Mwandishi: George Njogopa DW Dar es Salaam