1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaanzisha Kombe la Amani kwa albino

George Njogopa17 Machi 2015

Juhudi za kukabiliana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania zinapata nguvu mpya kupitia kampeni mbalimbali zinazolenga kuhamasisha jamii kupinga vitendo hivyo vya kinyama.

Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika shule ya msingi ya Mitindo.
Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika shule ya msingi ya Mitindo.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Pamoja na kampeni kadhaa zilizoanzishwa, siku ya Jumapili (tarehe 15 Machi) kulitarajiwa kuzinduliwa kampeni nyingine inayotumia kombe maalumu litakalozungushwa nchini kote kutuma ujumbe wa amani na kupinga mauaji ya albino.

Kampeni hii inazinduliwa katika wakati ambapo jeshi la polisi likitangaza kuwatia mbaroni zaidi wa waganga wa kienyeji 55 wanaotuhumiwa kupiga ramli zinazochonganisha watu ikiwamo zile zinazochochea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Hii ni kampeni ya kwanza inayotumia kombe maalumu ambalo litazungushwa katika maeneo mbalimbali hasa lakini katika eneo la kanda ya ziwa, eneo ambalo limekumbwa zaidi ya mauaji hayo.

Kampeni hii ambayo inawahusisha watu wa jamii zote, inaratibiwa na tasisi moja iloyojipa jukumu la kuwalea watoto walioko katika mazingira magumu na inafanywa kwa mfumo wa ushirikiano baina ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wale walioko katika hali ya kawaida.

Maisha ya allbino yalindwe

Mmoja wa waratibu wa kampeni hiyo alisema kuwa ujumbe mkubwa utakaozingatiwa wakati wote ni ule unasisitiza amani na kulinda maisha ya albino.

Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika shule ya msingi ya Mitindo.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Watu hawa wenye ulemavu ambao wamekuwa wakiishi katika hali ya wasiwasi na kihoro kikubwa, wanataka kuongezwa ulinzi hasa katika maeneo ya pembezoni ambako wimbi la matukio ya mauaji limeendelea kupamba moto.

Wanaamini kuwa kuanzishwa kwa kampeni za jinsi hii pamoja na msukumo kutoka kwa vyombo vya dola kutasaidia, kutaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza sokomoko hili.

Kijana huyu ambaye anaishi katika kituo cha kulelea watoto walioko kwenye mazingira magumu naye pia ni miongoni mwa hao wanaoamini kuwa kampeni hizo zinaweza kuzaa matunda.

Wito wa kimataifa

Kampeni hizi zinaanzishwa ikiwa siku chache tu baada ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuzika nchi za Afrika Mashariki kuongeza nguvu ya pamoja ili kukabiliana na vitendo vya mauaji ya albino.

Tayari vyombo vya dola vimefanikiwa kuwanasa wapiga ramli zaidi ya 55 wanaodaiwa kueneza chuki huku vikihaidi kuendelea kuwasaka wengine zaidi.

Serikali imesema pia itaendelea kushirikiana na watu wa kada mbalimbali ili kuhakikisha kwamba makundi ya watu wanaofanya ramli zenye uchonganishi wanadhibitiwa ipasavyo.

Kulingana na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paul Muhame, taasisi hiyo itaendelea kusimamia misingi yote inayoyohusu tiba za asili bila kuathiria jamii yoyote ya watu.

Waganga wa kienyeji na mara hii wanasiasa ni baadhi ya makundi yanayotajwa kuwa nyuma ya mauaji hayo yanayolaniwa duniani kote.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi

Onesha taarifa zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW