Tanzania yaendelea kukanusha uwepo wa Ebola nchini humo
3 Oktoba 2019Serikali ya Tanzania imeendelea kukanusha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo huku ikisisitiza kuwa, inakabiliwa na kitishi kikubwa dhidi ya ugonjwa huo ambao umegharibu idadi kubwa ya watu kwa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wizara ya afya nchini humo imesema katika sampuli zilizopimwa mwezi Septemba hazikuwa na maambukizi ya virusi vya Ebola.
Taarifa ya serikali imetolewa leo katika kipindi ambacho mataifa mbalimbali ikiwemo Uingereza yametoa tahadhari kwa watu wake walioko Tanzania na wale wanaotarajia kuingia nchini humo kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola baada ya taarifa za mwanamke mmoja kudaiwa kufariki na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewaambia wanahabari kuwa washukiwa wawili wa ugonjwa huo waliopimwa mwezi Septemba walithibitika kutokuwa na virusi vya Ebola na taarifa hizo ziliwasilishwa katika Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO ikiwa ni utaratibu wa kawaida.
Mwaka 2016 taifa hilo la ambalo lina muingiliano mkubwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Uganda ambapo katika mataifa hayo visa vya Ebola vimethibitishwa, lilikubali kufanyiwa tathmini ya utayari wa namna ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo na wataalamu kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni hatua ilioifanya Tanzania kujiimarisha zaidi hasa katika mipaka rasmi huku changamoto ikisalia katika mipaka isio rasmi ambayo inakadiriwa ni zaidi mia tatu.
Bado serikali ya Tanzania imeendelea kunyooshewa kidole na jumuia za kimataifa kutokana na kutokuwa na uwazi juu ya ugonjwa huo ikiwemo kutokubali kutoa sampuli ya vipimo vya watu waliohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi hivyo, ambapo serikali hiyo imesisitiza kuwa inafuata kanuni za kimataifa katika utoaji wa sampuli za vipomo vilivyobainika kuwa na virusi hivyo hatari huku ikishirikiana kwa ukaribu na WHO.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa hadi kufikia Septemba 30, jumla ya wagonjwa 3,194 walithibitishwa kuwa na maambukizi ya homa ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku wagonjwa 2,133 wakipoteza maisha ambayo ni sawa na asilimia 68. Mataifa yalio jirani na Kongo yameendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.