1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yajiandaa kwa uchaguzi Oktoba 28, 2020

26 Oktoba 2020

Watanzania wanaelekea kupiga kura Jumatano wiki hii katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa kipimo cha uvumilivu kwa mtindo wa uongozi wa Rais John Magufuli, anayeshutumiwa kuukandamiza upinzani na uhuru wa kujieleza. 

Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu

Taarifa zinaashiria kuwa katika wagombea wa urais 15, mpinzani mkuu wa rais Magufuli ni mgombea wa chama cha upinzani Chadema Tundu Lissu ambaye amerudi nchini Tanzania mwezi Julai baada ya kuishi ughaibuni kwa miaka 3 baada ya shambulizi linalodaiwa kuwa jaribio la mauwaji kisiasa.

Kurudi kwa Lissu kumeimarisha tena upinzani, baada ya kupigwa marufuku kwa mikutano ya kisiasa nje ya wakati wa uchaguzi, kukamatwa mara kadhaa na kushambuliwa hatua ambayo makundi ya kutetea haki za binaadamu wanatafsiri kama kufinya demokrasia.

Soma pia: Barua kutoka Dar: Hatua za lala Salama kuelekea uchaguzi

Katika kukuza nafasi za upinzani, Zitto Kabwe, mkuu wa chama  cha ACT-Wazalendo, mwezi huu alimuunga mkono Lissu kuwania urais Tanzania bara, akisema Lissu ana nafasi nzuri ya kumuondoa Rais Magufuli katika uchaguzi wa rais.

Chadema nayo inamuunga mkono mgombea mkongwe wa upinzani Seif Sharif Hamad katika azma yake ya sita ya urais Zanzibar, wakati huu dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Zanzibar imekuwa ikishuhudia ukosefu wa usalama na ghasia wakati wa uchaguzi lakini wakati huu kampeni zimeendeshwa kwa utulivu.

Kura ya maoni imepigwa marufuku nchini Tanzania hivyo haijulikani ni nani anayeongoza, na wasiwasi ni mkubwa juu ya matukio ambayo yanaweza kuharibu kura.

Mgombea urais wa chama cha CHADEMA, Tundu LissuPicha: Eric Boniphace/DW

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikionekana kama kimbilio la utulivu katika maeneo mengine yanayokubwa na vurugu, lakini hali imebadilika kuhusu uhuru tangu kuchaguzi kwa Magufuli mnamo 2015.

Pindi tu alipoingia madarakani Magufuli alifanya mabadiliko makubwa kama vile kuzuia kusafiri kwa maafisa wa serikali na muda mwengine kujitokeza kibinafsi kuhakikisha wafanyikazi wa umma wanafanya kazi zao kikamilifu.

Haukukomea hapo uongozi wa rais Magufuli ulipiga marufuku mikutano ya kisiasa, kuweka sheria kali kwa vyombo vya habari, kukamatwa kwa waandishi wa habari, wanaharakati na wanachama wa upinzani kupotea.

Rais Magufuli hata hivyo anajivunia mendeleo ya kuboresha elimu ya bure, umeme vijijini na miradi ya miundombinu kama reli, bwawa la kufua umeme lililowekwa kuongeza uwezo wa nchi wa kuzalisha nishati hiyo na ufufuaji wa shirika la ndege la kitaifa.

Serikali ya Magufuli pia ilipitisha msururu wa sheria za kuongeza hisa za Tanzania katika rasilimali zake za madini na kudai mamilioni ya dola kwa ushuru kutoka kwa kampuni za madini za nje.

Wachambuzi wa maswala ya kiuchumu wanahoji kuwa mbinu ya uongozi ya Magufuli imewatia wasiwasi wawekezaji.

Mwandishi: Saumu Njama

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW