1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura

21 Oktoba 2024

Kazi ya uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania imekamilika rasmi huku baadhi ya vyama vya upinzani vikilalamika kuwepo kwa mchezo mchafu katika mchakato huo.

Wananchi nchini Tanzania wakiwa tayari kujiandikisha katika daftari la wapiga kura
Wananchi nchini Tanzania wakiwa tayari kujiandikisha katika daftari la wapiga kuraPicha: Florence Majani

Uandikishaji huo ulianza Oktoba 11 na kumalizika Oktoba 20 umeshuhudia zaidi ya wananchi milioni 26 kote nchini wakijitokeza na kujiandikishawakiashiria kuwa tayari kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27.

Kwa mujibu wa Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ambaye wizara yake ndiyo inayoratibu uchaguzi huo, uandikishaji wa safari hii umevuka malengo na kwamba kiwango hicho cha waliojitokeza na sawa  na zaidi ya asilimia 81.

Kukamilika hatua ya uandikishaji wapiga kura kunaanza kutoa fursa kwa vyama vya siasa kuanzisha michakato ya ndani kwa ndani kuwarodhesha watia nia na kisha  kuwachuja kabla ya kuwafikisha kwa wapiga kura wakati wa uchaguzi wenyewe.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani vinavyotuhumu kuwepo kwa michezo michafu katika baadhi ya vituo vya kujiandikishia.Uchaguzi Tanzania: Wagombea wapiga kura

Wadau wa siasa nchini TanzaniaPicha: Florence Majani/DW

Sehemu ya tuhuma zao ni pamoja na kuoridheshwa kwa wapiga kura bandia, ukiukwaji wa kanuni za kuwaandikisha wapiga kura pamoja na kutokuwepo mifumo ya wazi katika kuwatambua wapiga kura hao.

Baadhi ya viongozi wa chama kikuu cha upinzani Chadema mkoani Katavi wanadaiwa kutiwa mbaroni na jeshi la polisi kutokana na hatua yao ya kuzusha malumbano katika kituo kimoja cha uandiikishaji wapiga kura. Viongozi hao walitia shaka juu ya mwenendo wa uandikishaji katika moja ya kituo vilivyopo wakilalamika juu ya ukiukwaji wa taratibu.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi limekuwa likiwasaka watuhukiwa kadhaa wanaodaiwa kuiba madaftari ya wapiga kura huko mkoani Kilimanjaro. 

Soma: Tanzania: Elimu ya mpiga kura kwa vijana yasisitizwa

Taarifa ya jeshi hilo haikuleza mazingira ya wizi huo mbali ya kusisitiza lipo kwenye ushirikiano na mamlaka nyingine kwa ajili ya kuwasaka wahusika wa tukio hilo. Tayari watuhumiwa kadhaa wanadaiwa kutiwa mbaroni.