1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakanusha kukandamiza uhuru wa habari

2 Agosti 2019

Licha ya ukosoaji unaoiandama kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, serikali nchini Tanzania imepuuzilia mbali hoja hiyo ikisema inawalinda vyema waandishi wa habari.

Harrison Mwakyembe
Picha: DW/E.Boniphace

Waziri wa Habari wa Tanzania, Harrison Mwakyembe, alisema wakati mwingine suala la uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia linakolezwa mno na mataifa ya Magharibi ambayo yanaona kwamba mataifa ya Kiafrika bado yako nyuma katika eneo hilo.

"Tanzania inaendelea kutambua na kuthamini sekta ya habari, hivyo kwa jinsi yoyote haiwezi kuweka mazingira ya kuvibana vyombo hivyo," alisema Mwakyembe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa (2 Agosti).

Waziri huyo ambaye mwenyewe ana uzoefu wa kufanya kazi za uandishi wa habari kabla ya kusomea sheria na kuingia kwenye siasa, alisema baadhi ya mataifa yamekuwa hodari kuionyooshea kidole Tanzania kuwa inabinya uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wake, "lakini ukweli wa mambo yenyewe ndiyo yenye rekodi mbaya kwa kuwa na idadi kubwa ya waandishi wananyanyaswa na hata wale wanaopoteza maisha."

Bado Erick Kabendera anashikiliwa

Kauli ya Waziri Makyembe, aliyekuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, inafuatia kuongezeka kwa wasiwasi miongoni mwa waandishi wa habari ambao baadhi wanahisi kuandamwa na mkono wa dola.

Hayo yanajiri katika wakati ambapo hatma ya mwandishi wa habari aliyekamatwa wiki iliyopita bado haijajulikana.

Duru za habari zinasema mwandishi huyo, Erick Kabendera, alikuwa akihojiwa na mamlaka za dola kuhusiana na uhalali wa uraia wake, huku watetezi wa haki za binaadamu wamekuwa wakipasa sauti kutaka mwandishi huyo aachiwe kwa dhamana. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alibanwa kuhusu baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumiwa na makundi ya watu ikiwamo wanasiasa kuwachafua wengine. 

Wakati huu ambapo Tanzania inajiandaa kuelekea katika uchaguzi mkuu kumekuwa kukishuhudia vyombo mbalimbali vikichukua mirengo mipya ambayo baadhi wanahisi ni kama maandalizi ya uchaguzi huo.
 

George Njogopa/DW Dar es Salaam

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW