1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakanusha kukatiwa misaada ya kifedha na Ulaya

Hawa Bihoga20 Novemba 2020

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ambaye pia ndiye mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya Jestas Abuok Nyamanga amesema si kweli kwamba Tanzania imekatiwa msaada wa kifedha wa zaidi ya shilingi trilioni moja.

Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Balozi Nyamanga amesema hayo kufuatia majadiliano yaliyofanyika katika bunge la Ulaya kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania ambapo wabunge kadhaa wa bunge hilo walielezea wasiwasi kuhusu hatma ya demokrasia huku wakiirai halmashauri kuu ya umoja huo kuzuwia misaada kwa taifa hilo.

Balozi Nyamanga amesema taarifa zinazoenezwa kwamba Tanzania imekatiwa msaada siyo za kweli, na kwamba kikao kilichofanyika siku ya Alhamisi kilikuwa cha kamati ya mambo ya nje yenye wabunge 71, na kati yao, ni watano tu waliochangia, na bado hawajafikia maazimio yoyote juu ya Tanzania.

Aidha, balozi Nyamanga amekanusha madai kwamba serikali ya Tanzania inapatiwa kiasi cha shilinigi trilioni moja kwa ajili ya kustawisha demokrasia kila mwaka kutoka Umoja wa Ulaya, akisisitiza kuwa Umoja huo una mashirikiano mazuri na Tanzania katika kuleta maendeleo.

"Si kweli kwamba fedha hizo zimesitishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali unaendelea , na hakuna azimio lolote la kusitisha fedha hizi. Na wanadai kuwa kuna majadiliano yanaendelea ya kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi, si kweli", alisema Balozi Nyamanga.

Zoezi la uchaguzi lililomalizika karibuni TanzaniaPicha: Ericky Boniphace/DW

Maoni mseto

Hata hivyo baadhi ya wadadisi wanasema ni vyema masuala muhimu yaliogusiwa kwenye mjadala huo yatolewe majibu stahiki na siyo kujitetea. Mmoja wa wachambuzi ambaye hakutaka kurekodiwa sauti, amesema Tanzania inapaswa kutoa majibu ya kimaandishi kwamba itaratibu uchaguzi huru na wa haki sambamba na kulinda demokrasia alioitaja kuwa imeporomoka kwa kiwango kikubwa.

Naibu Katibu mkuu wa chama cha Wananchi CUF kwa upande wa Tanzania bara Magdalena Sakaya, amesema anakubaliana na hoja zilizotolewa na wajumbe wa kamati hiyo ya bunge la Ulaya kuhusiana na kuporomoka kwa demokrasia, hivyo kuna haja ya kusubiria maazimio kamili, lakini amependekeza maazimio hayo yasiwe makali kiasi kwa kuwaathiri raia wa kawaida.

Ikiwa maazimio hayo yatahusisha vikwazo vya kiuchumi, yataathiri uwekezaji, pamoja na mauzo ya nje ya Tazania, kutokana na ukweli kwamba asilimia 17 mpaka 19 ya mauzo ya nje ya Tanzania yanafanyika katika Umoja wa Ulaya. Mchumi Bravious Kahzoza, anasema

"Ikiwa vikwazo hivi vinaweza kuwekwa matatizo ya aina hii ya uhusiano yanaweza kuwepo bila shaka kutakuwa na changamoto kubwa sana"

Katika majadiliano ya kawaida ya kamati ya mambo ya nje ya bunge la Ulaya, wajumbe wa kamati hiyo waliochangia walielezea wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, huku baadhi wakihoji kwa nini nchi hiyo iendelee kupewa fedha ya kusaidia dhidi ya athari za janga la COVID-19 wakati serikali ikisema tayari nchi hiyo imetokomeza ugonjwa huo.

Baada ya majadiliano kukamilika na kufikiwa maazimio, mapendeko yatapelekwa katika bumge la Ulaya kwa ajili ya kupitishwa rasmi ili yaanze kutekelezwa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW