Tanzania yakusanya silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria
17 Novemba 2021Waziri wa mambo ya ndani ya nchi George Simbachawene, amewaambia wanahabari kuwa zoezi hilo litaendeshwa nchi nzima kwa kipindi chote cha mwezi Novemba, na kwamba watu wote watakaowasilisha silaha wanazomiliki bila vibali watapewa msahama. Agizo hili la Tanzania ni utekelezaji wa makubaliano ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa ya mwaka 2018 kuhusu kudhibiti kuzagaa silaha haramu.
Akiwa jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania, waziri Simbachawene amewaambia wanahabari kuwa zoezi hilo limeanza rasmi tarehe mosi ya mwezi huu wa Novemba na kwamba watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe katika vituo vya polisi vya mikoa yao, na hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria. Serikali ya nchi hiyo inasema baada ya mwezi wa msamaha ambao ni mwezi huu wa Novemba kuisha, itaendesha msako mkali ili kuwabaini wote wanaomiliki silaha kiharamu na watachukuliwa hatuwa kwa mujibu wa sheria.
Zoezi hilo linaloendeshwa na Tanzania ni utekelezaji wa makubaliano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa yaliyofikiwa mwaka 2018 yanayohusu kudhibiti uzagaaji wa silaha haramu pamoja na kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Tanzania ikiwa mwanachama wa umoja wa mataifa, imewahi kuripoti visa kadhaa vya matukio ya uvunjivu wa amani vya kutumia silaha na hivyo serikali inasema zoezi litaendeshwa kwa umakini mkubwa.
Kabla ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika tayari zilikuwa zimefikia maazimio juu ya udhibiti wa silaha haramu katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika kuanzia tarehe Julai 2017 Jijini Addis Ababa Ethiopia, ambapo baraza hilo liliazimia kuutangaza mwezi Septemba kila mwaka kuwa ni mwezi wa usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari mpaka mwaka 2030, sambamba na kutoa msamaha kwa wahusika kutoshitakiwa endapo watasalimisha silaha hizo haramu kwa hiari na kwa muda uliopangwa.
Veronica Natalis DW, Arusha.