1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yasaini mkataba wa kuuza gesi yake asilia

12 Juni 2022

Tanzania imetiliana saini mkataba wa gesi na kampuni za Shell ya Uingereza na Equinor ya Norway ili kuutekeleza mradi wa dola bilioni 30 wa kuiwezesha nchi hiyo ya Afrika mashariki kuuza gesi yake asilia.

Strand in Mosambik - Anadarko
Picha: DW/Estácio Valoi

Kulingana na mkataba huo uwekezaji kwa ajili ya mradi huo utakamilishwa mnamo mwaka 2025 na kuanza shughuli kati ya mwaka 2029 na 2030 kwenye mtambo wa gesi ya kioevu utakaojengwa katika mji wa Lindi  kusini mwa Tanzania.

Hiyo ni hatua muhimu ya kusonga mbele kwa Tanzania  ya kuanzisha usafirishaji nje wa sehemu ya akiba kubwa ya raslimali hiyo iliyopo kwenye sehemu za pwani inayokadiriwa kufikia zaidi kubiki mita bilioni 1,630. Soma pia Mzozo wa gesi ya Mtwara

Waziri wa nishati wa Tanzania January Makamba amesema nchi hiyo haijawahi kufikia hatua kama hiyo ya maendeleo katika sekta ya gesi katika historia yake. Waziri Makamba amesema mradi huo utaubadilisha uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa.

Kijiografia, ni rahisi kwa Tanzania kusafirisha nje gesi asilia na hasa kwa nchi za bara la Asia zinazotafuta masoko mapya ya nishati.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwapo kwenye hafla ya kutia saini mkataba ameubariki mkataba huo wa kianzio. Rais Samia Hassan amesema hatua muhimu imefikiwa katika mazungumzo juu ya  mradi huo wa gesi asilia lakini ameeleza kuwa bado pana kazi kubwa ambayo Tanzania inapaswa kuifanya katika utekelezaji na kuipa Tanzania uwezo wa kushindana katika sekta ya gesi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Mipango juu ya mradi huyo ilisuasua wakati wa uongozi wa rais John Magufuli lakini rais Samia Suluhu Hassan aliuanzisha tena mradi huo baada ya kuingia madarakani.

Meneja wa kampuni ya Equinor ya Norway kanda ya Tanzania Unni Fjaer amesema mkaba uliofikiwa umefanyiwa kazi kwa muda mrefu. Ameeleza kuwa kazi ilisimama simama lakini kutokana na ari ya kusonga mbele, mazungumzo yaliendelea na amesema kuwa sekta ya gesi ya Tanzania inatoa fursa maridhawa.

Kampuni za Marekani ExxonMobili na ya Equinor ya Norway zimearifu kuwa zimegundua kubiki mita trillioni 20 za gesi asilia kwenye pwani ya Lindi, kusini mwa Tanzania. Nazo kampuni za Shell na Ophir Energy zimesema zimegundua kubiki mita trillioni 16 za gesi asilia kwenye maeneo ya karibu.Mkutano wa Wadau wa sekta ya mafuta na gesi mjini Arusha,Tanzania

Sawa na nchi nyingi duniani uchumi wa Tanzania pia uliathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na janga la corona. Hatua za kudhibiti maambukizi zilikatiza mapato yanayotokana na shughuli za utalii, ambayo ni sekta muhimu inayoiingizia Tanzania mapato makubwa.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW