1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Tanzania yasema makusanyo ya kodi bado yako chini

27 Februari 2024

Serikali ya Tanzania imesema kuna haja ya kutoa elimu ya kina kuhusu utayari wa kulipa kodi, ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi sambamba na kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Tanzania I Dar es Salaam
Jiji la Dar es Salaam linachangia pakubwa katika mapato ya serikali ya Tanzania.Picha: Pond5/IMAGO

Ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi Tanzania ni chini ya asilimia 12 ya pato la taifa hali inayochochewa na mwamko mdogo wa ulipaji kodi wa Watanzania katika wakati ambao nchi nyingine za Afrika zikiwa na asilimia ya juu ya makusanyo ya kodi.

Ni katika muktadha huu, ndipo Makamu wa Rais Dk. Philip Isdory Mpango alipozitaka mamlaka, taasisi na asasi zinazoshughulika na masuala ya ukusanyaji wa fedha kuendelea kutoa elimu ya ulipaji wa kodi.

''Kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wawekezaji wa nje na wa ndani, kwa mujibu wa TNBC wafanyabiashara na wawekezaji wamekuwa wakilalamikia mambo kadhaa ikiwamo utitiri wa kodi, sera za kodi, rushwa, viwango vya juu vya kodi,'' alisema Dr. Mpango.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.Picha: Presidential Press Service Tanzania

Soma pia: Afrika: Wataalamu wakubaliana kuimarisha mifumo ya kodi

Mpango aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema ukusanyaji mdogo wa kodi unachangia hali mbaya ya uchumi na akataka mamlaka husika kufanya jitihada za kukusanya kodi angalau kwa asilimia 15 ya pato la taifa.

Kiwango hiki ni chini ya wastani wa asilimia 15.6 ya zaidi ya pato la taifa kwa nchi za Afrika.

Alisisitiza kufanyika kwa maboresho ya sheria, sera na viwango vya kodi, kuendelea kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji sambamba na kupunguza viwango vya ushuru wa forodha.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba alisema changamoto kubwa katika sekta hiyo ni ulipaji wa kodi kwa hiyari na utoaji wa risiti ambapo amesema, wafanyabiashara wamekuwa vinara wakiwaongoza wanunuzi kukwepa kodi.

Mwaka 2023 Shirika la Sikika nchini Tanzania lilitoa ripoti yake kuhusu sababu za wafanyabiashara kutokulipa kodi, na utafiti huo uliainisha mambo kadhaa ikiwamo utitiri wa kodi, mlolongo mrefu wa mchakato wa ulipaji kodi na wakusanyaji wa kodi kutumia nguvu wakati wa kukusanya kodi.

Soma pia:Makampuni ya kigeni yalalamikia kodi kubwa Tanzania 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo alisema kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Jukwaa la kodi kwa mwaka huu liliongozwa na kaulimbiu isemayo; maboresho ya sera katika uwekezaji na ukusanyaji wa mapato ya ndani na ukuaji wa uchumi jumuishi. 

Viongozi wa kimataifa waliohudhuria jukwaa hilo ni pamoja Rais wa Mabunge Duniani  na Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson, mawaziri, viongozi wa asasi za uwekezaji na uchumi Tanzania.