1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: yasema wagombea wa upinzani wanaweza kukata rufaa

11 Novemba 2024

Kilio cha vyama vya upinzani nchini Tanzania kuhusu kuchezewa rafu katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa kimechukua sura mpya baada ya vyama hivyo kulalamika kushindwa kuweka pingamizi.

Uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania
Picha: Florence Majani

Kilio cha vyama vya upinzani nchini Tanzania kuhusu kuchezewa rafu katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa kimechukua sura mpya baada ya vyama hivyo kulalamika kushindwa kuweka pingamizi mara baada ya ofisi za watendaji na wasimamizi wa uchaguzi kufungwa  huku wagombea wa upinzani walioteuliwa awali, majina yao yakienguliwa.

Soma pia: Joto la kisiasa lapanda kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania

Hata hivyo, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, imedai kuwa malalamiko ya wapinzani yameletwa wakati zoezi la kuweka pingamizi limeisha, lakini kwa sasa wanaweza kukata rufaa. 

Vilio bado vimetawala. Hivyo ndivyo tunavyoweza kusema baada ya vyama vya upinzani nchini, kulalamika kufungwa kwa ofisi za wasimamizi na watendaji wa uchaguzi, ambako wagombea walioenguliwa kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa walitakiwa kuweka pingamizi huku likizuka wimbi jipya ambapo Chadema kimedai, wagombea wao walioteuliwa awali, wameenguliwa. 

Hatua ya vyama vya upinzani kuweka pingamizi ilikuja baada ya vyama hivyo kulalamika wagombea wao  kuenguliwa katika hatua ya kuteuliwa kuwania nafasi katika uongozi wa serikali za mitaa. 

Soma pia:Tanzania yakamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura 

Chama cha upinzani cha Chadema kimedai, wagombea wao walioteuliwa awali, wameenguliwaPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Novemba 8 mwaka huu Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alivitaka vyama vya upinzani kuwaelekeza wagombea walioenguliwa kuweka pingamizi kati ya Novemba 9 na 10.

Hata hivyo, Katika taarifa yao kwa umma waliyoitoa Novemba 9, CHADEMA walilalamika kuwa ofisi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambako ndiko wagombea walitakiwa Kwenda kuweka pingamizi, zilikuwa zimefungwa na hivyo wagombea wao wakashindwa  kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza na DW, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema licha ya wagombea kushindwa kuweka pingamizi, limezuka wimbi jipya.

Mrema amesema,  kama chama, kinasubiri kuona ni wagombea wangapi wa CHADEMA waliobaki kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa kisha kitafanya tathmini na kueleza umma namna uchaguzi huu uliovyoendeshwa.

Akizungumza na DW, Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI, Adolph Ndunguru, amesema malalamiko ya wapinzani yamekuja wakati zoezi la pingamizi limeshafungwa lakini zoezi la rufaa bado linaendelea. Na hapa anaongeza zaidi.

Kadhalika Ndunguru amewataka wapinzani waseme wazi ni ofisi ipi ya serikali iliyofungwa wakati zoezi hili la rufani likiendelea ili wao Tamisemi, walishughulikie.

Uchaguzi wa serikali za mitaa katika taifa hili la Afrika Mashariki unafanyika unafanyika mnamo Novemba 27, katika mazingira ambayo hayapishani sana na ule wa mwisho wa mwaka 2019, ambapo chama kinachotawala CCM kilijizolea takribani viti vyote, kutokana na wagombea wa upinzani kushindwa kuwania kwa sababu zinazofanana na hizi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW