1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yathibitisha kifo cha mwanafunzi alietekwa na Hamas

Hawa Bihoga
14 Desemba 2023

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania leo Alhamisi ilithibitisha kifo cha mmoja wa raia wake ambaye "aliuawa mara baada ya kukamatwa na Hamas" wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 kusini mwa Israel.

Tanzania | Rais Samia Suluhu
Rais wa Tanzania samia Suluhu HassanPicha: AP/picture alliance

Serikali ya Israel iliwataja wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao ni  Clemence Felix Mtenga mwenye umri wa miaka 22 na Joshua Loitu Mollel mwenye umri wa miaka 21, miongoni mwa waliotoweka tangu shambulio hilo.

Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania ilitangaza kifo cha Mtenga mwezi uliopita, bila kueleza jinsi alivyouawa.

Waziri wa Mambo ya Nje January Makamba alisema mamlaka "imearifiwa na serikali ya Israel kwamba Joshua Mollel, kijana wa Kitanzania aliyekuwa akisoma nchini Israel na ambaye tumepoteza mawasiliano naye tangu Oktoba 7, 2023... aliuawa mara baada ya kukamatwa na Hamas".

Soma pia:Israel imeendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa yanayotaka isitishe mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza

Kupitia mtandao wa X Waziri Makamba alisema kuwa mamlaka za Tanzania zinafanya utaratibu wa ndugu wa Mollel akiwemo baba yake kusafiri hadi Israel na afisa wa serikali ili "kukutana na balozi wetu na maofisa wa Israel na kupata maelezo zaidi" juu ya mazingira ya kifo chake.

Wanafunzi hao wawili walikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda Israel kwa ajili ya mafunzo ya ukulima wa kisasa chini ya mpango wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Maeneo yalioathiriwa na shambulio la Hamas Israel

Maeneo mengi yaliyoathiriwa zaidi na mashambulizi ya Hamas yalikuwa ni jumuiya za kilimo za Israel, ambazo zinapakana na eneo linalopakana na Ukanda wa Gaza.

Wanamgambo wa Hamas wanaoorodheshwa kama magaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya Ujerumani ikiwemo na mataifa mengine, waliivamia Israel mnamo Oktoba 7 na kuua takriban watu 1,200 -- wengi wao wakiwa raia -- kulingana na mamlaka ya Israeli, na kuwakamata takribani mateka 240.

Israel na Hamas wameanza tena mapigano

00:56

This browser does not support the video element.

Hamas iliwaachilia huru makumi ya mateka badala ya wafungwa wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa na Israel wakati wa mapatano ya wiki moja mwezi uliopita, lakini wengine waliuwawa kwa mujibu wa wafuatiliaji.

Soma pia:Nani atafadhili ujenzi mpya wa Gaza, karibu nusu ya majengo yake yamebomolewa au kuteketezwa kabisa

Israel imeapa kuwaangamiza Hamas kwa kampeni ya ardhini, angani na baharini huko Gaza.

Vita hivyo vimesababisha kuzingirwa kwa Gaza na kuwa magofu na kuua zaidi ya watu 18,600, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.