Tanzania yazinduwa safari za majaribio za treni ya umeme
26 Februari 2024Majaribio hayo yalifanyika siku ya Jumatatu (Februari 26) wakati mradi huo ukiwa umekamilika wa zaidi ya asilimia 98, ikiashiria uwekezano wa kuanza shughuli zake rasmi.
Hadi sasa, tayari Shirika la Relila nchi hiyo (TRC) limepokea jumla ya mabehewa 62 vichwa vinne vya umeme.
Mabehewa mengine pamoja na vichwa vyake yalikuwa yanatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi wa Machi.
Kuanza kwa majaribio hayo kulimaliza uvumi wa muda mrefu kuhusu kusuasua kwa mradi huo ambao majaribio yake mengine yatakayofikisha hadi mji mkuu, Dodoma, yalikuwa yanatarajiwa kuanza katika miezi ya karibuni.
Soma zaidi: Tanzania na Burundi zasaini makubaliano ya ujenzi wa reli
Kipande cha reli kutoka Morogoro hadi Dodoma kinaripotiwa kuwa kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 95.
"Majaribio haya ni hatua mojawapo ya mwisho kuelekea kuanza rasmi safari zake ifikapo mwezi Julai." Alisema Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa.
Habari njema kwa Tanzania na majirani zake
Kukamilika kwa mradi huo ni habari njema kwa wananchi wengi wanaoona kwamba utawapughuzia adha ya usafiri hasa wakati huu ambako matumizi ya barabara yamekuwa na changamoto kubwa ikiwemo vizuizi vinavyosababoishwa na askari wa usalama barabarani.
"Mabasi ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yamekuwa yakitumia muda wa masaa manne hadi matano, wakati usafiri wa treni ya umeme hutumia muda usiozidi masaa mawili tu." Mmoja wa abiria aliyekuwamo kwenye treni hiyo aliiambia DW.
Soma zaidi: Tanzania yatenga ardhi kwa Zambia kujenga bandari kavu
Msemaji wa serikali, Mobahare Matinyi anaamini kwamba mapinduzi ya usafiri wa treni yameiva rasmi. "Kuna uwezekano wa kuendelea kupokea mitambo mingine zaidi ya treni," aliongeza.
Mradi huo wa treni ya umeme ulitazamiwa pia kuwa habari njema kwa nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, ambazo hutegemea bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirishia mizigo yake.