1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzia: Maisha ya Rais Daniel Arap Moi

Daniel Gakuba
4 Februari 2020

Rais wa zamani wa Kenya, Daniel Arap Moi amefariki dunia tarehe 04.02.2020 akiwa na umri wa miaka 95. Bendera zote nchini mwake zinapepea nusu mlingoti, na Rais Uhuru Kenyatta ameahidi atapewa mazishi yenye heshima zote.

Kenia 1992 | Daniel Arap Moi, ehemaliger Präsident
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

 

Wakenya walimpa jina la utani la ''mwenye kirungu'', Daniel Toroitich Arap Moi, rais wa pili wa Kenya aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 24 kuanzia 1978 hadi 2002. Kifimbo alichotembea nacho kila mahali, ni ishara ya uongozi katika jamii yake ya Kalenjin.

Moi alizaliwa tarehe 2 Septemba 1924 katika kijiji kidogo cha Kurieng'wo katika mkoa wa Bonde la Ufa. Jina la Toroitich linamaanisha, mwana wa mchungaji wa ngombe. Baba yake alifariki Moi akiwa na umri wa miaka minne, akalelewa na mjomba wake alimsaidia kusoma hadi kuhitimu na kupata stashahada ya ualimu.

Daniel Arap Moi alikuwa miongoni mwa Wakenya wachache walioteuliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Majimbo la serikali ya wakolini wa kiingereza mwaka 1955.

Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo KenyattaPicha: Imago Images//United Archives International

Yeye hakushiriki moja kwa moja katika vuguvugu la Mau-Mau lililochukua silaha kupigania uhuru wa Kenya mnamo miaka ya 1950, lakini alimuunga mkono kiongozi wa vuguvugu hilo, Jomo Kenyatta, na alimtembelea alipokuwa gerezani.

Kuunganisha vyama

Moi alikuwa mwanachama wa chama cha KADU (Kenya African Democratic Party), tofauti na Jomo Kenyatta aliyekuwa katika chama cha KANU (Kenya African National Union). Aliunga mkono sera ya kuwa na utawala wa kimajimbo, huku pia akijikita katika kutetea maslahi ya jamii yake ya Kalenjin na makabila mengine madogo katika taifa la Kenye lenye makabila mengi. Kwa upande mwingine, Jomo Kenyatta alitoka jamii ya Wakikuyu ambao ndio wengi nchini Kenya.

Baada ya uhuru wa Kenya mwaka 1963, Kenyatta alimshawishi mpinzani wake Moi kuunganisha vyama vyao, ukawa mwanzo wa utawala wa chama kimoja. Moi alipata nafasi katika serikali ya Kenyatta, akiwa waziri wa mambo ya ndani. Mwaka 1967, Kenyatta alimteuwa Moi kuwa makamu wake, licha ya upinzani mkali wa wasomi kutoka jamii yake ya Wakikuyu. Kenyatta alifariki mwaka 1978 akiwa na umri wa miaka 84, na Moi akarithi kiti chake.

Wapiganaji wa Mau Mau waliupa wakati mgumu utawala wa Wakoloni WaingerezaPicha: Getty Images

Mwaka uliofuata, urais wa Moi ulithibitishwa katika uchaguzi, ambapo alisimama kama mgombea pekee. Mwaka 1982, aliidhinisha utawala wa chama kimoja katika katiba ya Kenya.

Ukandamizaji dhidi ya wapinzani

Tofauti na mtangulizi wake, Daniel Arap Moi alikuwa karibu na wananchi, akifanya ziara katika maeneo mengi ya Kenya. Wakati huo huo lakini alikuwa akifanya kila njia kuwapendelea watu wa jamii yake ya Kalenjin kwa vyeo na mali. Ukandamizaji wa uhuru wa habari ilikuwa mojawapo ya nembo za utawala wake.

Kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka 1982, Moi alizidisha utawala kwa mkono wa chuma. Jaribio hilo la mapinduzi la wanajeshi wa kikosi cha anga lilifuatiwa na ukandamizaji mkubwa, ambamo zaidi ya watu 120 waliuawa, na wengine zaidi ya 900 wakawekwa kizuizini. Watu 12 waliokutwa na hatia ya kuhusika katika jaribio hilo walihukumiwa kifo.

Marehemu Dr Robert Ouko, mhanga wa utawala wa Rais MoiPicha: imago/Sven Simon

Lakini pia Moi aliwachukulia hatua kali wakosoaji ndani ya chama chake, akimtuhumu waziri wa sheria Charles Mugane Njonjo kufanya uhaini. Baada ya kesi mahakamani, Njonjo alilazimika kujiuzulu mwaka 1983, akishutumiwa kutaka kuuangusha utawala wa Moi. Mhanga mwingine wa mkono wa Moi ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Robert Ouko aliyeuawa kikatili mwaka 1990, baada ya kukosoa waziwazi matumizi mabaya ya madaraka na kutaka uchunguzi ufanywe dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Baada ya miaka 10 ya uchunguzi wa kamati ya bunge, ilibainishwa kuwa Ouko aliuliwa katika makaazi ya Rais Moi. Wakati wa uchunguzi huo, mashahidi kadhaa walikufa katika mazingira ya kutatanisha, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya kamati hiyo. Wapinzani wengine walioonja machungu ya utawala wa Rais Daniel Arap Moi ni Kennath Matiba na Raila Odinga, ambao walifungwa jela bila kufikishwa mahakamani.

Hatimaye akubali shinikizo, arejesha mfumo wa vyama vingi

Shinikizo kali la kimataifa lilimlazimisha Moi hatimaye kuridhia mfumo wa vyama vingi mwaka 1991. Mwaka 1992, Wakenya walipata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi uliovihusisha vyama vingi, lakini upinzani uliogawanyika ulikuwa neema kwa Moi, ingawa ilikuwepo pia minong'ono ya kughushi matokeo. Uchaguzi huo uliandamwa na machafuko makubwa.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, alifungwa bila kufunguliwa mashtakaPicha: Reuters/T. Mukoya

Miaka mitano iliyofuata, Moi alishinda tena. Ingawa sehemu kubwa ya Wakenya iliunga mkono upinzani wapizani hao walishindwa kukubaliana juu ya mwakilishi mmoja wa kambi yao.

Mwaka 2002 Moi alikosolewa vikali pale alipojaribu kuahirisha uchaguzi wa bunge kwa sababu ya mazungumzo juu ya katiba mpya, akiwa na azma ya kuendelea kukaa madarakani. Kikatiba alikuwa haruhusiwi kugombea tena, na uchaguzi ulifanyika kama ilivyopangwa. Alisababisha pia mvutano mkali ndani ya chama chake kwa kumchagua mtoto wa mtangulizi wake, kijana Uhuru Kenyatta ambaye hakuwa na uzoefu, kama mgombea wa chama cha KANU.

Mkakati wake wa kutaka KANU iungwe mkono kwa sababu mgombea wake alitoka jamii ya Wakikuyu walio wengi uliambulia patupu, na ilichukua miaka mingine 11 kwa Uhuru kuingia Ikulu.

Utawala wa miaka 24 wa Daniel Toroitich Arap Moi ulifika kikomo tarehe 30 Desemba 2002. Urithi aliouacha wa ukabila na ubadhirifu unaiandama Kenya hadi wa leo.

dw

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW