1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tatizo la huduma za afya mashariki mwa Ukraine

Josephat Nyiro Charo3 Februari 2015

Watu waliotengwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata huduma msingi za afya katika eneo la Ukraine linalokabiliwa na vita. Eneo hilo liko katika hatari ya kutumbukia kwenye mzozo mkubwa wa kibinaadamu.

Ukraine Protest Arzneimittel Mangel HIV Klinik in Kiew
Picha: Reuters

Mzozo kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na vikosi vya Ukraine umewaathiri watu zaidi ya milioni tano, huku milioni 1.4 kati yao wakiorodheshwa na shirika la afya duniani, WHO, na mashirika ya kutetea haki za binaadamu kuwa wanakabiliwa na kitisho kikubwa kwa sababu ya kulazimika kuyakimbia makazi yao, ukosefu wa kipato na kusambaratika kwa huduma muhimu, zikiwemo za afya.

Mapigano pamoja na hatua zilizochukuliwa na pende husika katika mzozo huo zimesababisha mahitaji ya dawa kutatizwa kwa kiwango kikubwa au kukatika kabisa, hospitali zimeharibiwa au kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maji na umeme, na uhaba wa wafanyakazi katika vituo vya afya huku maafisa wa afya wakiyakimbia mapigano.

Kukosekana kabisa chanjo kunatishia kutokea miripuko ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kupooza na surua. Kuna wasiwasi miongoni mwa watu wanaoishi na ugonjwa hatari wa ukimwi na kifua kikuu, huku usafirishaji wa dawa muhimu ukikwama kabisa na juhudi za kufuatilia magonjwa zikiwa karibu haziwezekani.

Mashambulizi mjini DonetskPicha: Menahem KahanaAFP/Getty Images

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na mgogoro wa mashariki mwa Ukraine ni 700,000, ambao sasa wamegeuka kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Idadi hiyo inasemekana inaongezeka kwa 100,000 kila wiki huku mamia kwa maelfu wakiishi katika hali ngumu za kukatisha tamaa na mazingira machafu yasiyo salama kwa kuishi, hivyo kusababisha kitisho cha afya na fursa kwamba magonjwa ya kuambukiza kama kifua kikuu yatasambaa.

Changamoto ya kuzifikia huduma za afya

Huku kukiwa na kitisho kwa utoaji wa huduma za afya mashariki mwa Ukraine kutokana na kusambaratika kwa raslimali, baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wanakabiliwa na vikwazo vya ziada vya kufikia huduma za afya.

Ukraine ina mlipuko mbaya kabisa duniani wa ugonjwa wa ukimwi na kuenea kwa ugonjwa huo kumechochewa kwa kiwango kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya kutumia sindano. Hata hivyo tofauti na mataifa mengine ya Mashariki mwa Ulaya, nchi hiyo imekuwa ikiendesha kwa muda wa zaidi ya muongo mmoja programu kadhaa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ambazo zimepongezwa kimataifa kwa kudhibiti kuenea kwa ukimwi.

Programu hizi zimekuwa zikitolewa kote Ukraine na ni muhimu sana katika eneo la mashariki kwa sababu idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya kutumia sindano wanatokea maeneo ya Luhansk na Donetsk mashariki mwa nchi hiyo.

Dawa za kuwaokoa watumiaji dawa la kulevya ni habaPicha: picture alliance/JOKER

Lakini mashirika ya kitaifa na kimataifa yanayofanya kazi kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya yanasema upatikanaji wa huduma za kuyaokoa maisha katika maeneo hayo umekabiliwa na shinikizo tangu ulipoanza mzozo na kwamba huenda ukakatizwa kabisa katika wiki chache zijazo, huku usafirishaji wa dawa zinazotumiwa katika matibabu, methadone na buprenorphine, zikiisha na haziwezi kupelekwa huko.

Waroma hawapati huduma na wanabaguliwa

Kundi lengine la watu wanaotengwa na wanaopata shida kupata huduma za afya ni jamii ya Waroma. Kihistoria inakadiriwa jamii ya Waroma takriban 400,000 nchini Ukraine, kama Waroma wengine katika nchi za Ulaya Mashariki, zinakabiliwa na ubaguzi mkubwa katika jamii, ikiwemo katika masuala ya ajira na elimu. Wamekuwa hawapati huduma za matibabu kwa sababu wengi hawana vitambulisho rasmi, hali inayoifanya vigumu kwa Waroma wengi kupata huduma za afya, huku umaskini uliokithiri ukiwa na maana huduma na dawa zinazohitaji kulipiwa haziwezi kuwafikia.

Dr Dorit Nitzan, Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, ofisi ya Ukraine ameliambia shirika la habari la IPS "Hata kabla mzozo kuanza, Waroma nchini Ukraine walikuwa wakizifikia huduma chache za matibabu ya afya na za kukinga magonjwa. Matokeo yake watoto wengi wa Waroma hawajapata chanjo. Pamoja na hayo kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza iko juu miongoni mwa Waroma, ikilinganishwa na umma jumla wa Ukraine."

Ubaguzi pia ni tatizo. Zola Kondur wa shirika la Waroma la haki za binaadamu la Chiricli ameliambia shirika la habari la IPS kuwa Waroma ni miongoni mwa watu wanaokabiliwa na hatari nchini Ukraine na wanafanyiwa ubaya kwa sababu ya kabila lao.

Mwandishi: Josephat Charo/IPS

Mhariri:Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi