Tatizo la njaa barani Afrika
12 Agosti 2005Taasisi hiyo inayochunguza masuala ya chakula imesema iwapo hakuta kuwa na mabadiliko ya sera basi hali itazidi kuwa mbaya. Tayari mamilioni ya watu wamekumbwa na upungufu wa chakula katika nchi zinazopakana na jangwa la Sahara.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka taasisi hiyo, bara la Afrika linahitaji kiasi cha dola bilioni 303 za kimarekani katika uwekezaji kulisaidia kuondokana na tatizo la njaa.
Bwana Mark Rosegrant, mwandishi mmoja wapo wa ripoti hiyo, amesema uwekezaji kama huo utaweza kupunguza idadi ya watoto wenye lishe duni latika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara hadi kufikia milioni 10.
Akizungumza na wandishi wa habari aliongeza kwamba itakuwa vizuri zaidi ikiwa viongozi wa mataifa matajiri wataongeza kwa mara mbili idadi ya misaada na viongozi wa nchi za Afrika waongeze kwa mara mbili idadi ya uwekezaji kwenye kilimo. Pia matokeo yatakuwa bora kama viongozi hao wa Afrika wataimarisha mipango ya kilimo, ardhi na maji.
Pia uchunguzi kutoka Umoja wa Mataifa umeonyesha kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara ndio sehemu pekee katika maeneo yenye nchi zinazoendelea ambyo hali ya upungufu wa chakula imekuwa ikiongezeka kwa kipindi cha takriban miaka 30.
Matokeo yake ni Afrika itashindwa kufikia malengo ya mellenium. Malengo hayo yalikuwa na nia ya kupunguza kwa nusu umaskini duniani, ifikapo mwaka 2015.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana inaeleza kwamba haitakuwa jambo la kushangaza kwa watu kwamba Afrika haitaweza kutimiza malengo hayo.
Maeneo mengine yenye nchi zinazoendelea kama Kusini-Mashariki mwa bara la Asia hali ni tofauti. Eneo hilo limeweza kupambana vyema na tatizo la lishe duni, hasa miongoni mwa watoto.
Afrika ina matatizo kutokana na mfumo wa kilimo. Kuna uongozi mbaya wa kisiasa na kiuchumi wa kilimo, pia uwekezaji kwenye sekta hii ni wa kiasi cha chini na hamna mfumo bora wa unyesheaji wa mazao. Sekta hii pia haifanyiwi utafiti na uchunguzi ipasavyo.
Matatizo mengine yanayo ikumba bara hilo ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya chakula. Afrika inashindwa kwa sababu ya hali ya hewa, mazingira na hali duni ya kifedha.
Pia matatizo mengine ya kijamii yanachangia yakiwemo madhara yaliosababishwa na ugonjwa wa UKIMWI, umaskini, kutokuwepo na usawa baina ya jinsia na wanawake kutopewa nafasi katika jamii.
Tatizo la kupatikana kwa maji pia linachangia.
Mwezi uliopita wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari kwenye Umoja wa Mataifa, rais wa baraza la masuala ya kiuchumi na kijamii, Balozi wa Pakistani, Munir Akram, alisema tatizo linalozidi kila siku la madeni ya nchi zinazoendelea linazuia juhudi za kupambana na umaskini na njaa Afrika.
Kwa mujib wa Balozi Akram jumla ya madeni ya nchi za Afrika ni dola trilioni moja za kimarekani, bilioni 40 zimesamehewa hivi karibuni na mataifa ya magharibi.
Aliongeza kwamba kusamehewa kwa madeni hyo kutapunguzia mzigo mkubwa kwa nchi 18. Lakini bado kuna mataifa mengine 30 ambayo yanasumbuka na madeni.
Naye Bwana Rosegrant, mwandishi wa ripoti ya taasi ya kimataifa, akizungumza na shirika la habari la IPS alisema kuwa wasiwasi kama nchi zilizosamehewa madeni zitapata mafanikio kama watatumia vizuri fedha hizo katika sekta ya kilimo na suala la kuhifadhi chakula.
Ripoti hiyo iliuliza swali moja kuu nalo ni; Je kuna uwezekano kwa Afrika kufanikisha malengo ya mellennium ya kupunguza njaa na umaskini kwa nusu?
Baadhi ya mapendekezo kutoka ripoti hiyo ni kufanywa mageuzi ya sera za biashara za kimataifa na uwekezaji uzingatiwe kwenye miundo mbinu ya vijijini, elimu na masuala ya kijamii.
Pia usimamizi wa nafaka, ardhi na maji ni lazima uboreshwe. Bara la Afrika litakapoweza kuendeleza uzalishaji ndio litakapoweza kuwa na akiba nzuri ya chakula na uwekezaji katika utafiti wa kilimo uongezwe.