1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tawala za Mashariki ya kati na teknolojia ya akili bandia

23 Agosti 2023

Tawala za kimabavu katika nchi za Mashariki ya Kati hutumia utambulisho ulioboreshwa kwa kutumia vifaa vya akili bandia vya kibaiometriki kuwafuata wapinzani wao.

Roboti
Roboti linalotumia teknolojia ya akili bandiaPicha: Bastian/Caro/picture alliance

Mnamo mwezi Mei mwaka huu, Khalaf al-Romaithi alisafiri kwa ndege kutoka Uturuki hadi Jordan kutafuta shule mpya kwa ajili ya mtoto wake. Lakini mpinzani huyo wa Emarati aliwekwa kizuizini sababu ikiwa ni macho yake. Au, kuwa sahihi zaidi, ni kwa sababu ya taarifa za biometriki zilizokuwemo kwenye macho yake.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 58 alikuwa akisafiri kwa kutumia pasipoti ya Uturuki, lakini taarifa kwenye mboni za yake kwenye uwanja wa ndege wa Amman zilionyesha ni Khalaf al-Romaithi yuleyule aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hiyo ni sehemu tu ya kesi kubwa iliyowakabili wakosoaji 94 wa uongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu mnamo mwaka 2013, ambayo mashirika ya haki za binadamu yamelaani kuwa ilichochewa kisiasa.

TeknolojiaPicha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

Mtu huyo alizuiliwa katika uwanja wa ndege wa Amman baada ya uchunguzi wa mboni za macho yake alithibitisha Hamad al-Shamsi, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalosaidia wafungwa katika magereza ya UAE. Ameongeza, kusema kwamba hakuna mtu aliye na uhakika jinsi Wajordan walivyopata data za kibayometriki za al-Romaithi.

Si wawakilishi wa Jordan au wa Emarati hapa nchini Ujerumani waliojibu maombi ya DW ya kutaka maoni yao kuhusu suala hilo.

Kulingana na wanasheria, Al-Romaithi ameondolewa kinyume cha sheria kutoka Jordan na kupelekwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambako ametiwa gerezani.

Jinsi gani serikali zitadhibiti teknolojia ya akili bandia?

Kesi ya al-Romaithi ni ishara ya kutia wasiwasi linapokuja suala la jinsi taarifa za kibinafsi za kibayometriki zinavyotumika katika nchi za Mashariki ya Kati, ameelezea Yana Gorokhovskaia wa shirika la kutetea demokrasia la Freedom House lenye makao yake makuu nchini Marekani.

Ameiambia DW kwamba wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya kibayometriki kuwezesha ushirikiano wa karibu kati ya serikali kandamizi, jambo ambalo wamelishuhudia katika nchi za Mashariki ya Kati na pia katika nchi za Asia ya kati.

Wageni wakitembelea banda la Huawei katika mkutano wa teknolojia DubaiPicha: Mahmoud Khaled/picture alliance

Taasisi ya Ulaya inayoshuguhulikia maswala ya Mediterania, imethibitisha kwamba matumizi makubwa ya mifumo ya utambulisho wa kibayometriki, pamoja na sheria dhaifu za faragha na sheria dhaifu za ulinzi wa haki za binadamu, hufungua mlango kwa ukiukaji mkubwa wa binadamu, ambapo zana zinazotumia akili bandia zinaweza kuzidisha, hali hiyo kimabavu dhidi ya binadamu, wamesema waandishi wa utafiti wa mwaka 2022 kuhusu sera ya akili bandia katika Mashariki ya Kati.

Mataifa tajiri katika eneo hilo, kama vile nchi za Ghuba, yanapendelea utambuzi wa kibayometriki. Mohammed Soliman, mkurugenzi wa mpango wa kimkakati wa teknolojia na usalama wa mtandao katika Taasisi ya Mashariki ya Kati yenye makao yake mjini Washington, ameiambia DW kwamba teknolojia hizi ni za msingi kwani kanda hii hasa nchi za Ghuba zinapitia mabadiliko ya kidijitali.

UN kufanya mkutano kuhusu teknolojia ya akili bandia.

Hivi sasa, karibu nchi zote za Mashariki ya Kati hutumia taarifa za kibayometriki katika viwanja vya ndege na mipakani. Dubai imesema teknolojia hiyo imeleta mafanikio baada ya polisi kwenye uwanja wake wa ndege kumnasa tapeli mmoja, ambaye alitumia kadi bandia kwa kuangalia sura na masikio yake. Katika kesi nyingine, walimkamata mwanamume aliyekuwa amevalia gauni refu la kike na kujifunika uso kutokana na jinsi anavyotembea na vipimo vya mwili wake.

Kuongezeka kwa matumizi ya akili bandia Goma

02:38

This browser does not support the video element.

Hata hivyo wataalamu wanasema taarifa hizo zinaweza  kutumika kwa njia mbaya. Taasisi ya akili bandia ya AI Now inataka utambulisho wa kibayometriki upigwe marufuku. Amba Kak, mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya AI Now yenye makao yake mjini New York, Marekani ameiambia DW kwamba sheria za faragha na sheria zingine hazitasaidia. Ameongeza kusema kuwa sio tu katika Mashariki ya Kati, lakini hata nchini Marekani na Ulaya pia. Matatizo ya mifumo hii hayatatatuliwa kwa haraka katika demokrasia huria ya nchi za Magharibi ingawa kinyume chake kile kinachoweza kwenda vibaya mara nyingi huonekana upesi kwenye nchi zinazotawaliwa kimabavu.

Mhariri: Jacob Safari

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW