1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tawi la chama cha AfD Ujerumani lawekwa chini ya uchunguzi

12 Machi 2020

Idara ya upelelezi wa ndani nchini Ujerumani BfV inalichunguza kundi la itakadi kali linalojulikana kama Fluegel, lililoasisiwa na Chama AfD, kwa madai ya kuendeleza siasa kali na mashambulizi dhidi ya wageni.

Björn Höcke
Picha: picture-alliance/dpa/B. Schackow

Fluegel au bawa ni tawi la itikadi kali la chama cha AfD linaloongozwa na Bjoern Hoecke, kiongozi wa chama  hicho katika jimbo la Thuringia. Akizungumza mjini Berlin, Mkuu wa idara ya upelelezi wa ndani BfV, Thomas Haldenwang, amesema Hoecke na Andreas Kalbitz, anaekiongoza chama hicho katika bunge la jimbo la Brandenburg, wamethibitishwa kuwa  wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia.

Hoecke pamoja na wanachama wengine wa chama hicho wanadaiwa kutoa kauli za kupitiliza zilizotumika wakati wa enzi za wanazi. Hoecke pia anajulikana kwa kauli zake dhidi ya Uislamu na wahamiaji. 

Idara hiyo ya upelelezi wa ndani, maarufu kama ofisi ya shirikisho ya ulinzi wa katiba, tayari imekuwa ikilifuatilia kundi la Fluegel pamoja na tawi la vijana la AfD tangu Januari mwaka 2019 kwa shaka za itikadi kali za mrengo wa kulia. Idara hiyo ilithibitisha shaka hizo na kupandisha hadhi ya Fluegel hadi kesi ya kuchunguzwa, hii ikimaanisha kwamba watoa taarifa wanaweza kujipenyeza katika kundi hilo, na pia serikali kukusanya taarifa kuhusu baadhi ya watu.

AfD yazidi kupata wafuasi

BfV inaamini kundi la Fluegel lina wafuasi 7000 katika kundi lisilo rasmi lakini lililojipanga vizuri. Hata hivyo, msemaji wa chama cha AfD katika jimbo la Thuringia Stefan Moeller amesema anaamini kile kinachoendelea ni njama ya kukichafulia sifa na kukivunjia imani kwa wanachama wake. 

Pamekuwa na maandamano mara kwa mara kupinga AfDPicha: picture-alliance/dpa/S. Wurtscheid

Katika miaka michache chama cha AfD kinachowapinga wahamiaji kimekua kutoka chama kidogo hadi kufikia chama kikubwa cha upinzani katika bunge la taifa. Moeller amesema siasa za AfD haziendi kinyume na katiba na kutilia shaka namna idara ya upelelezi wa ndani inavyoweza kufuatilia kundi la Fluegel. 

Serikali ya Ujerumani awali iliapa kukabiliana na siasa za itikadi kali za mrengo wa kulia kufuatia mashambulizi kadhaa dhidi ya wageni yaliotokea nchini humo. Shambulizi la hivi karibuni ni lile la mjini Hanau karibu na Frankfurt ambako mtu aliyejihami kwa bunduki aliwauwa raia tisa wa kigeni kabla ya kumuua mamake na yeye mwenyewe pia kujitoa uhai. 

Mshambuliaji huyo hakuwa na mafungamano na kundi la AfD, lakini vyama kadhaa vya kisiasa vilikilaumu chama hicho kwa kauli za kuujaza chuki umma dhidi ya raia wa kigeni. 

Chanzo: afp/ap/reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW