TBILISI: Urusi yaiwekea vikwazo Georgia
3 Oktoba 2006Georgia imewaachilia huru maofisa wanne wa jeshi la Urusi waliokuwa wakizuiliwa kwa kushukiwa kuwa makachero. Lakini Urusi iliyokasirishwa na hatua hiyo ya Georgia, imeiwekea vikwazo nchi hiyo ikitaka kuiadhibu, uamuzi ambao huenda uwe pigo kubwa kwa Georgia ambayo uchumi wake bado unayumbayumba.
Wapatanishi wa mataifa ya magharibi wameishawishi Urusi iwache malumbano baada ya Georgia kuwaachilia maofisa wake katika kile ilichokiita kitendo cha kirafiki. Lakini Urusi imepuuza ushauri huo na imesema kuanzia leo itakatiza usafiri wa reli, angani na baharini na huduma za posta na Georgia.
Kukamatwa kwa wanajeshi wa Urusi na maofisa wa usalama wa Georgia kumedhihirisha hali ya wasiwasi iliyopo baina ya nchi hizo mbili. Georgia inataka kujiunga na shirika la NATO na Umoja wa Ulaya, jambo linaloitia wasiwasi Urusi ambayo inaiona Georgia kama sehemu ya eneo inalolidhibiti.