Ted Cruz amwangusha Trump katika mchujo wa Iowa
2 Februari 2016Ted Cruz ameshangiriwa na umati wa wafuasi wake katika jimbo la Iowa, baada ya mgombea huyo mwenye mrengo mkali wa kihafidhina katika chama cha Republican kushinda uchaguzi wa mchujo katika jimbo hilo, akimpita Donald Trump kwa asilimia zaidi ya tatu ya kura zilizopigwa. Cruz ambaye aliungwa mkono na wafuasi wa madhehebu ya walokole alipata asilimia 27.7, akifuatiwa na Donald Trump aliyepata asilimia 24, na katika nafasi ya tatu, yupo mgombea kijana, seneta wa jimbo la Florida Marco Rubio mwenye asilimia 23.
''Ushindi hautaamliwa na vyombo vya habari''
Akiwahutubia mashabiki wake baada ya kutangazwa mshindi katika mchujo huo, Ted Cruz aliashiria kukejeli kura za maoni zinazomuonyesha mpinzani wake mkubwa, bilionea Donald Trump akiongoza katika kinyang'anyiro cha chama cha Republican kitaifa, akisema wapiga kura ndio wanaoamua.
''Usiku huu, ni ushindi kwa wahafidhina jasiri katika jimbo la Iowa, na kwingineko katika taifa hili kubwa'', amesema Cruz na kuongeza kuwa Iowa imetuma ujumbe, kwamba mgombea wa chama cha Republican na rais wa Marekani anayefuata, hatachaguliwa na vyombo vya habari.
Trump ambaye kwa muda mrefu amejijengea sura ya kiongozi wa mbio hizo za mchujo ndani ya chama chake, amesema anaona fahari kuwa katika nafasi ya pili, lakini wachambuzi wanasema matokeo haya yataitia doa sura hiyo aliyoijenga.
Hillary Clinton amponyoka Bernie Sanders
Kwa upande wa chama cha Democratric, uongozi wa kampeni ya Hillary Clinton umetangaza ushindi wa mgombea wao. Takwimu za awali zilimuonyesha Bi Clinton akikaribiana sana na mpinzani wake mkuu Bernie Sanders, kila mmoja wao akipindukia asilimia 49 ya kura zilizopigwa katika jimbo hilo la Iowa.
Katika hotuba aliyoitoa mbele ya kambi yake alfajiri ya leo Jumanne, Clinton amezungumzia mikakati atakayoipa kipaumbele.
''Najua tunaweza kuboresha elimu kwa watoto wetu wote, hususan wale wenye matatizo, najua baada ya kuungwa mkono na vijana tunaweza kuipunguza gharama ya kusoma chuo kikuu na kuwapa wanafunzi mikopo, najua kwamba tunaweza kulinda haki za wote, wanawake, mashoga,..na pia najua kuwa tunaweza kuweka sheria nzuri za umiliki salama wa bunduki.' Amesema kwa hamasa Bi Clinton.
Wengine wafungasha virago
Baada ya matokeo haya, baadhi ya wagombea wameamua kufungasha vyao na kuziaga mbio hizo za urais. Gavana wa zamani wa jimbo la Maryland Martin O'Malley kutoka chama cha Democratic ameaziaga mbio hizo baada ya kuambulia patupu katika uchaguzi wa mchujo wa jimbo la Iowa. Kwa upande wa chama cha Republican, aliyekuwa gavana wa jimbo la Arkansas Mike Huckabee pia ameamua kukiaga kinyang'anyiro baada ya kupata kura zisizofika asilimia mbili.
Katika chama cha Republican, Ben Carson amekuja katika nafasi ya nne, seneta Rand Paul katika nafasi ya tano, naye gavana wa zamani wa Florifa Jeb Bush akajikuta katika nafasi ya sita katika uchaguzi huo wa mchujo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe
Mhariri:Yusuf Saumu