1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tedros ateuliwa kuwa mgombea pekee kuendelea kuongoza WHO

25 Januari 2022

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO ana uhakika wa kuiongoza taasisi hiyo kwa muhula wa pili baada ya kupigiwa kura inayomfanya kuwa mtu pekee atakayegombea uchaguzi wa wadhifa huo mwezi Mei

Genf, Schweiz | 74. WHO-Jahrestagung | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Laurent Gillieron/Keystone/picture alliance

Tedros Adhanom Ghebreyesus amabye ni kiongozi wa kwanza Mwafrika wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa ameshukuru kwa uungwaji mkono alioupata, baada ya bodi ya utendaji ya WHO kupiga kura ya siri iliyoidhinisha uteuzi wake wa kuwa mgombea pekee kwa wadhifa huo.

Tedros, mmoja wa viongozi waliogonga vichwa vya habari katika mapambano ya kimataifa ya janga la COVID-19, alikiri kuwa muhula wake wa kwanza wa miaka mitano ulikuwa na changamoto na mgumu na akasema ni heshima kubwa kupewa fursa ya kuendelea kupambana.

Waziri huyo wa zamani wa Afya na mambo ya nje wa Ethiopia anatarajiwa kuchaguliwa  bila wakati mataifa yote 194 wanachama wa WHO yatapiga kura zao kumchagua Mkurugenzi Mkuu mwezi Mei

Tangu kuanza kwa janga la COVID 19 duniani miaka miwili iliyopita, Tedros aliye na miaka 56 na mtaalamu wa ugonjwa wa Malaria amepokea sifa nyingi kwa namna alivyoiongoza dunia katika mapambano ya janga hilo.

Mataifa ya Afrika yamefurahishwa na umakini unaotolewa kwa bara hilo kutokana na kampeni ya Tedros  ya kuyasaidia mataifa masikini kupata chanjo  dhidi ya COVID 19.

soma zaidi:WHO yakemea kukosekana kwa usawa katika usambazaji wa chanjo

Ethiopia yataka Tedros achunguzwe kwa kuliunga mkono kundi la TPLF

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Hata hivyo upinzani wa Tedros umekuja kutoka taifa lake. Serikali ya Ethiopia imepuuzilia mbali matamshi yake juu ya hali ya mgogoro wa kibinaadamu katika eneo la Tigray katika vita vilivyodumu miezi 14.

Mwanzoni mwa mwezi huu Tedros aliifananisha hali katika eneo hilo kuwa sawa na jehanamu na kuituhumu serikali ya Ethiopia kuzuwiya madawa  na msaada mwengine kufika katika maeneo yaliyoathirika. 

Kutokana na matamshi hayo Ethiopia ikataka achunguzwe kwa madai ya  kuhusika na hatua za kuunga mkono vikosi vya wapiganaji wa Tigray wanaopambana na serikali kuu ya Ethiopia.

Hata hivyo Mwenyekiti wa bodi kuu ya utendaji ya WHO Patrick Amoth amearifu kwamba taasisi hiyo itaakhirisha kutowa uamuzi kuhusu ombi lililotolewa.  Amoth amesema ombi la serikali ya Ethiopia ni suala gumu lenye kubeba athari za kisiasa  na liko nje ya mfumo wa taratibu za kamati hiyo na kupendekeza suala hilo liwekwe kando,na kujadiliwa na wale wanaohusika katika wakati mwafaka.

Chanzo: afp/ap


      
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW