TEHRAN: Maafisa wa Iran wakutana na wajumbe wa shirika la IAEA
20 Agosti 2007Maafisa wa Iran wanakutana leo na wajumbe wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, kwa raundi ya tatu ya mazungumzo mjini Tehran baadaye leo.
Mkutano huo utajadili ombi la Iran kuwa wazi zaidi kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, kama sehemu ya juhudi za kuzuia azimio la tatu la vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi yake.
Rais George W Bush wa Marekani amesema sera yake inalenga kuizuia Iran isiwe na uwezo wa kutengeneza silaha za kinyuklia.
´Sera yetu ni kuwazuia wasiwe uwezo wa kurutubisha uranium kufikia kwiango cha kuweza kutengeneza silaha ya nyukilia´
Iran inatarajia shirika la kimatiafa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuuklia lizungumzie kwa kina ushirikiano wa Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia katika ripoti yake ya mwezi ujao, ambayo itaamua ikiwa Iran ikabiliwe na vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa au la. Mikutano mingine miwili kati ya Iran na shirika la IAEA ilifanyika mwezi uliopita na mwanzoni mwa mwezi huu.
Naibu kiongozi wa shirika la nishati ya nyuklia nchini Iran, Mohammed Saeedi, ameyaeleza mazungumzo ya leo kuwa muhimu lakini akadokeza kuwa itachukua muda mrefu kabla makubaliano kufikiwa.