Teknolojia ya "kuvuna maji ya mvua" yasaidia nchini Kenya
13 Agosti 2007Chini ya mlima unaoitwa Uvilio, wanawake na watoto wanapiga foleni wakisubiri mitungi ya kubebea maji ijazwe. Bei ya maji kwa mtungi mmoja wa lita ishirini ni Shilingi mbili za Kenya. Mapato yanatumika kuendesha kituo hiki ambacho kimejengwa na shirika la kijerumani la kupiga vita njaa duniani, “Welthungerhilfe”. Mkuu wa mradi huu, Peter Njoroge, anaonyesha vile kuta ndogo ndogo zilivyojengwa ndani ya mawe. Anasema: “Tunatumia umbo la nje la mawe kukusanya maji. Mvua ikinyesha tunayaelekeza maji kwa kutumia teknolojia rahisi sana na kuyakusanya katika bwawa na tangi kubwa la maji.”
Jina maalum la teknolojia hii ni “Rainwater Harvesting”, yaani kuvuna mvua. Ni teknolojia ya zamani ya kukusanya maji ya mvua na kutumia maji kwa muda mrefu. Kwenye mlima wa Uvilia kuna matangi manane ya maji yanayoweza kuchukua lita laki tisa za maji. Haya yanaweza kuwatosheleza wakaazi wanaoishi karibu na mlima huu kwa muda wa mwaka moja.
Kulingana na mradi la Umoja wa Mataifa unaohusika na mazingira, UNEP, matumizi ya mvua kama chanzo cha maji ni fursa nzuri kwa nchi kama Kenya. Katika utafiti uliochapishwa hivi karibuni, wataalamu wamegundua kuwa kiwango cha mvua nchini Kenya ni mara sita au saba zaidi kuliko mahitaji ya maji ya wakaazi wote wa nchi hiyo.
Shirika la Kijerumani la “Welthungerhilfe” hivi sasa linatafuta mahala pa kujenga vituo vingine vya kuvuna mvua. Kama Martin Kessler anayeendesha mradi huo alivyoeleza, ushirikiano na wakazi wa Makueni ulikuwa mzuri sana na watu wengi walijitolea katika kazi ngumu ya ujenzi.
Hiyo ndiyo sababu nyingine ya kuendelea na mradi huo, anasema Martin Kessler: “Kwa maoni yetu, kuna nafasi nyingi nzuri katika eneo la Kusini Mashariki mwa Kenya. Katika wilaya hizo mbili ambapo tunafanya kazi kuna milima 30 ambayo inafaa kutengenezwa kama vituo vya kukusanya mvua, lakini hatujaichunguza milima yote. Kwa hivyo ninakaridiria kwa ujumla kuna milia 60 au hata 100 ambayo inapaswa kutumika kwa ajili hiyo.”
Wakati hali ya hewa inabadilika na mvua haiwezi kutegemewa, mabwawa na matangi ya maji yatakuwa na umuhimu mkubwa.