Teknolojia Yaiangusha Kenya katika Uchaguzi
7 Machi 2013Watu 1,200 waliuwawa kufuatia uchaguzi uliofanyika miaka mitano iliopita.Kuhesabiwa pole pole kwa kura kunauweka mfumo wa teknolojia ya kuhesabu kura katika mtihani barani Afrika.Utowaji wa matokeo kwa mwendo wa konokono baada ya kushindwa kwa mfumo wa elektroniki uliotumika kutuma idadi ya kura kutoka vituo vya kupigia kura moja kwa moja hadi kituo kikuu cha kuhesabia kura kumezidisha hali ya mashaka ya wapiga kura na yumkini kukadhoofisha matumaini yanayowekewa mifumo ya aina hiyo kutumika katika chaguzi nyengine barani Afrika.
Chaguzi zilizopita nchini Kenya zimegubikwa na kura hewa,kujazwa kwa kura za bandia kwenye visanduku vya kupigia kura na udanganyifu wakati wa kuhesabu kura mambo ambayo yamekuwa yakisibu chaguzi katika eneo zima la kusini ya jangwa la Sahara barani Afrika kwa miongo kadhaa wakati viongozi waliotopea rushwa wakipuuza matawaka ya wananchi.Katika uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2007 wapinzani walidai kuwa umehujumiwa wakati rais anayeeondoka madarakani Mwai Kibaki aliposhinda kwa kipindi cha pili na kuitumbukiza nchi hiyo yenye nguvu kubwa za kiuchumi Afrika Mashariki kwenye machafuko.
Safari hii Kenya imenuwia kuwa na mchakato wa uchaguzi wa kuaminika na wa wazi.Bitange Ndemo mtumishi mwandamizi wa serikali wa wizara ya habari na mawasiliano ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba amefadhaishwa kwamba mchakato huo umeshindwa kufanya kazi.Amesema kompyuta zilizotumiwa na tume ya uchaguzi kushughulikia data zinazoingia zimeelemewa.
Katika siku ya uchaguzi zaidi ya nusu ya mashine zenye kusoma alama za vidole za kuwatambuwa wapiga kura zimeharibika kwenye vituo vya kupigia kura nchini kote na kuwalazimisha maafisa kutumia makaratasi ya usajili.Baya zaidi mfumo wa elektroniki wa kurusha matokeo ambao ni muhimu kwa ajili ya kuwasilisha kwa haraka matokeo ulikabiliwa na vikwazo vilivyopelekea kuwepo kwa ombwe la matokeo jambo ambalo limezusha aina fulani ya nadharia za njama ambapo serikali ilikuwa imefanya kila njia kuliepuka.Pia imetowa fursa kwa wagombea hasimu kuwa na mashaka na kuaminika kwa matokeo hayo.
Wakati matokeo ya awali yakitiririka kupitia mfumo wa kutowa matokeo kupitia simu za mkono Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ilianza kutowa matokeo ya awali wakati maafisa wa uchaguzi walipoanza kuwasili Nairobi kutoka vituo vya kupigia kura vilioko mbali kabisa.Kampuni ya Safaricom ambayo hutowa huduma za mawasiliano ya simu imesema mifumo yake inafanya kazi lakini matatizo yamezuka kutokana na zana ambayo haiwajibiki nayo.
Afrika imekuwa ikitumia simu za mkono na teknolojia nyengine kukabiliana na mapungufu katika sekta ya miundo mbinu.Kenya yenyewe imekuwa ikitumia simu za mkono kwa huduma za benki teknolojia ambayo imekuwa ikitumika kuanzia bara la Asia hadi Amerika Kusini.Kenya sio nchi ya kwanza kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika kukabiliwa na matatizo hayo ya teknolojia itakumbukwa kwamba uchaguzi wa rais nchini Ghana hapo mwaka 2012 uliongezwa muda hadi siku ya pili baada ya mashine za kusajili wapiga kura zilizokuwa zikitumiwa kwa mara ya kwanza kushindwa kufanya kazi katika zaidi ya vituo 400 kati ya vituo 26,000 vya kupigia kura.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri: Yusuf,Saumu