TEL AVIV : Israel yaondowa vikwazo vyake Lebanon
9 Septemba 2006Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steimeir ameulezea uamuzi wa Israel kuondowa vikwazo vya baharini kwa Lebanon kuwa ni hatua muhimu.
Katika mkutano wake mjini Tel Aviv na waziri wa Ulinzi wa Israel Amir Peretz Steinmeir pia amesema Ujerumani iko tayari kusaidia katika jitihada za kufanikisha kuachiliwa kwa wanajeshi wawili wa Israel waliotekwa nyara na Hizbollah hapo mwezi wa Julai.
Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon amesema manowari za Ufaransa,Italia na Ugiriki hivi sasa zinapiga doria kwenye mwambao wa Lebanon.
Wanamaji hao wanatarajiwa kupiga doria kwenye mwambao wa Lebanon kuzuwiya silaha zisiwafikie Hizbollah hadi hapo manowari za Ujerumani zitakapochukuwa nafasi zao rasmi katika kipindi cha wiki mbili au tatu zinazokuja.