1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ten Hag alalamikia kipigo cha Arsenal

4 Septemba 2023

Arsenal imeiadhibu Manchester United kipigo cha 3-1 kunako dakika za lala salama ndani ya uga wa Emirates huku Kocha wa United Erik ten Hag akighadhabishwa na matokeo hayo.

Fußball I Erik ten Hag
Picha: Zac Goodwin/empics/picture alliance

Ilionekana kama mechi hiyo ingekamilika kwa sare ya 1-1 lakini The Gunners kupitia wachezaji Declan Rice na Gabriel Jesus walisambaratisha matumaini ya United.

Awali mchezaji Alejandro Garnacho wa Manchester United alitia kimyani bao dakika ya 88 lakini baada ya uangalizi wa mfumo wa Video wa VAR ilionekana kaotea, uamuzi ambao kocha Ten Hag hakukubaniana nao.

Soma pia: Manchester United yamsaini Onana kwa mkataba wa miaka mitano

Ten Hag alikosa maamuzi ya refa wa mechi hiyo ikiwa ni pamoja na tukio la beki wa Arsenal, Gabriel, kumchezea rafu mchezaji mpya Rasmus Hojlund ambaye kwa maoni yake ingefaa kuwa penalti.

Baada ya kichapo hicho Ten Hag amesema; "Tuanzie kwa adhabu iliyopaswa kutolewa. Kila mtu alimuoona Kai Havertz akipiga mbizi, Kisha kumfanyia madhambi Hojlund, kwenye eneo la hatari. Hata haikuonekana na mwamuzi msaidizi. Kisha, bao lililokataliwa kutoka kwa Garnacho. Nadhani, video ya VAR haikutazama vizuri, ukiangalia kwa pembeni ungeona ni bao. Na kisha goli la mwisho... Wanaweza kuruhusu bao hilo?

United inakwenda kwenye mapumziko ya kimataifa ikiwa na pointi sita katika jumla ya mechi nne.

Katika ligi ya Uhispania La Liga, Barcelona hapo jana ilipata ushindi mgumu wa 2-1 dhidi ya Osasuna.  Mchezaji Jules Kounde alitia kimyani bao la kwanza kwa Barcelona lakini Chimy Avila aliisawazisha kabla ya kukamilika kipindi cha kwanza.

Robert Lewandowski alipata penalty baada ya kuchezewa vibaya na Alejandro Catena ndani ya kisanduku hatua ambayo ilimsabishia kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Robert Lewandowski Picha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Mechi ya Atletico Madrid dhidi ya Sevilla iliahirishwa kwa utabiri wa hali ya hewa kutarajia mvua kubwa katika mji mkuu wa Uhispania, ingawa mvua iliyotabiriwa haikutokea katika muda ambao mchezo huo uliratibiwa.

Soma pia: Bellingham atulia vyema Madrid

Viongozi wa Ligi Real Madrid waliilaza Getafe 2-1 siku ya Jumamosi ndani ya uga wa Santiago Bernabeu,  Huku mchezaji wa zamani wa Borussia Dortmund Jude Bellingham akiendelea kutamba baada ya kufunga bao lake la tano kati ya mechi nne.