1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko jingine la ardhi Nepal lazidisha maafa

13 Mei 2015

Idadi ya waliofariki katika tetemeko la ardhi Nepal lililotokea hapo jana imepita watu 80 huku visa vya maporomoko ya ardhi vikiendelea kuripotiwa katika taifa hilo ambalo lilikumbwa na tetemeko jingine hivi karibuni.

Picha: picture-alliance/epa/N. Shrestha

Maelfu ya watu waliojawa na hofu nchini Nepal wamekesha nje ya nyumba zao usiku wa kuamkia leo wakihofia maafa zaidi kufuatia tetemeko jingine la kiwango cha 7.3 katika kipimo cha Ritcher ambalo liliziathiri pia India na China.

Helikopta ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa imewabeba wanajeshi wanane wa majini wa Marekani na wanajeshi wawili wa Nepal imeripotiwa kutoweka ilipokuwa ikisambaza misadaa hapo jana kaskazini mwa Nepal katika mji wa Dolakha.

Ndege ya Marekani haijulikani iliko

Maafisa wa Nepal na Marekani wamesema uchunguzi umeanzishwa kuitafuta ndege hiyo. Hata hivyo mpaka sasa hakuna ishara kuwa imeanguka na inahofiwa huenda ilitua katika eneo ambalo hakuna mawasiliano. Wengi wa walioathirika na tetemeko hilo jipya ni kutoka Kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Kathmandu.

Wanajeshi wambeba muathiriwa wa tetemeko la ardhiPicha: Reuters/N. Chitrakar

Mkuu wa wilaya ya Dolakha Prem Lal Lamichane amesema watu wamejawa na hofu kila sehemu na waliamua kulala katika maeneo yaliyo wazi usiku na kuongeza wameanza kuishiwa misaada ya kibinaadamu. Narayan Prasad raia wa Nepal anasema amepoteza kila kitu.

Lamichane ameiomba serikali kutuma helikopta zaidi za misaada kwani kuna majeruhi wengi waliokwama katika vijiji kadhaa. Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Nepal, kiasi ya watu 2,000 wamejeruhiwa lakini kulingana na ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa idadi ya waathirwa inatarajiwa kupanda kwani kuna ripoti watu na vijiji vya milima ya Himalaya wamezikwa chini ya vifusi.

India na China pia zaathirika

Katika taifa jirani la India, takriban watu 16 wamethibitishwa kuuawa katika jimbo la Bihar lililoko kusini mwa mpaka na Nepal baada ya paa na kuta za nyumba kuwaangukia kutokana na kishindo cha tetemeko hilo la ardhi. China imeripoti mtu mmoja ameuawa katika eneo la Tibet.

Mwanamke alia nje ya hospitali ya Kathmandu nchini NepalPicha: Getty Images/J. Gratzer

Nepal imeomba msaada wa mabilioni ya dola kutoka kwa mataifa ya kigeni pamoja na wataalamu wa afya kuwatibu waliojeruhiwa na helikopta za kusafirsiha vyakula na mahema kwa maelfu ya raia wake walioachwa bila ya makaazi kufuatia maafa hayo.

Maafisa wa shughuli za uokozi pia wanawatafuta manusura wa janga la jana katika majengo yaliyoporomoka katika mji wa Chautara ulioko katika wilaya ya Sindupalchowk ambao umekuwa kitovu cha kutolewa misaada ya kibinadamu tangu tetemeko la kwanza la ardhi lililotokea tarehe 25 mwezi jana.

Mwandishi: Caro Robi/ap/dpa

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW