1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Tetemeko la ardhi lasababisha vifo vingi Uturuki na Syria

6 Februari 2023

Zaidi ya watu 600 wamekufa na maelfu wengine wamejeruhiwa, baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter, kupiga katikati mwa Uturuki na Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Türkei Diyarbakir Erdbeben
Picha: IHA/AP Photo/picture alliance

Naibu Rais wa Uturuki Fuat Oktay, amesema zaidi ya watu 284 wamekufa na wengine zaidi ya 2,300 wamejeruhiwa katika mkasa huo, huku akisema bado vikosi vya waokoaji vinaendelea kuwatafuta manusura zaidi waliokwama chini ya majengo yaliyoporomoka.

Nchini Syria, taifa ambalo tayari limesambaratika kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 11, afisa mmoja wa serikali katika kitengo cha afya, amesema zaidi ya watu 237 wamekufa huku zaidi ya 600 wakijeruhiwa.

Afisa huyo amesema mikoa mengi kama ya Hama, Aleppo na Latakia yameharibiwa vibaya kwa tetemeko hilo kufuatia majengo mengi kuporomoka.  Rais wa Syria Bashar al Assad yupo katika mkutano wa dharura na Baraza lake la mawaziri kujadili hatua zaidi za kuchukuliwa kufuatia taifa kukumbwa na mkasa huo mkubwa.

Tetemeko hilo kubwa lililokuwa na ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter, lilisikika pia nchini Cyprus na Lebanon.

Watu zaidi waokolewa chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka

Timu ya waokoaji wakijaribu kuwaokoa manusura chini ya vifusi vya majengi yaliyoporomoka Kusini Mashariki mwa UturukiPicha: AP Photo/picture alliance

Televisheni ya taifa nchini Uturuki RTR imewaonyesha timu ya waokoaji katika mkoa wa Osmaniye wakitumia blanketi kuwabeba manusura wa mkasa huo. Huku hayo yakiarifiwa ofisi ya rais Tayyip Erdogan wa Uturuki, imesema kiongozi huyo yupo katika mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia ya simu na magavana wa majimbo 8 yaliyoathiriwa vibaya kujua juhudi zaidi zinazofanyika za kuwaokoa watu waliokwama chini ya majengo yalioanguka.

Watu 100 waokolea Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi

Wakati uo huo, Umoja wa Ulaya kupitia  Kamishna wa idara inayoshughulikia mizozo katika Umoja huo Janez Lenarcic umeamua kutuma timu ya waokoaji na kutoa usaidizi zaidi kwa Uturuki baada ya tetemeko hilo lililosababisha mauaji ya watu wengi. Timu kutoka uholanzi na Romania tayari zipo njiani kuelekea Uturuki.

Ujerumani iko pamoja na Uturuki na Syria katika wakati huu mgumu

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Kira Hofmann/photothek/IMAGO

Kwa upande mwengine Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba Ujerumani inawaombea familia na watu waliopoteza maisha yao katika tetemeko hilo, na wale ambao bado wanaohofu wasiojua walipo jamaa zao, marafiki na hata majirani.

Baerbock amesema Ujerumani ikiwa pamoja na washirika wake iko tayari kutoa msaada, tamko lililoungwa mkono pia na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz.

Jake Sullivan, mshauri wa ikulu ya Marekani kuhusu Usalama wa taifa, amesema wanafuatilia kwa karibu kinachoendelea Uturuki na Syria na wako tayari pia kutuma msaada wa haraka. Ufaransa pia kupitia rais wake Emmanuel Macron imetoa ujumbe sawa na huo.

Tetemeko la ardhi laua Uturuki

Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikikumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara, ambapo mwaka 1999 watu 17,000 walikufa kutokana na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Ritcha lilipoupiga mji wa Izmit na na mwaka 2011 tetemeko jengine likaupiga mji wa Van na kusababisha vifo vya watu 500

Mwandishi: Amina Abubakar/reuters/ap/afp

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW