Tetemeko la ardhi laua Uturuki
25 Oktoba 2011Matangazo
Mpaka sasa watu wasiopungua 275 wamekufa kutokana na tetemeko hilo lililoikumba sehemu ya mashariki mwa Uturuki ambako watu wamelazimika kulala nje kwa siku ya pili katika baridi kali. Waokoaji wanaotumia taa zinazotumia nguvu za majenereta na zana zingine nzito, wameendelea kuwatafuta walionusurika katika mji wa Ercis uliokumbwa vibaya sana na maafa ya tetemeko.
Huduma za maji na umeme zimekatika katika mji huo kutokana na tetemeko. Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alieutembelea mji wa Van, ambako tetemeko la ardhi lilianzia amesema takriban nyumba zote zilizojengwa kwa matofali ya udongo zimesambaratika katika vijiji vinavyouzunguka mji huo. Taarifa zaidi zinasema mitetemeko mingine zaidi ya 200 ilifuatia.