1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Tetemeko la ardhi laua zaidi ya watu 1,000 Morocco

Angela Mdungu
9 Septemba 2023

Zaidi ya watu 1,000 wamefariki dunia baada ya tetemeko la ardhi kutokea nchini Morocco Ijumaa usiku. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imesema watu wengine zaidi ya 1,200 wamejeruhiwa katika janga hilo.

Marokko Hunderte Tote bei schwerem Erdbeben
Picha: Fadel Senna/AFP/Getty Images

Tetemeko hilo lenye ukubwawa 6.8 kwenye kipimo cha Richter, limesababisha uharibifu wa majengo katika vijiji vya milima ya Atlas hadi kwenye mji wa kihistoria, Marrakech.

Wengi wa waliokufa ni kutoka katika mikoa mitano iliyo karibu na eneo lililoathiriwa zaidi na tetemeko hilo. Idadi ya vifo na majeruhi inatarajiwa kuongezeka wakati waokoaji wakifukua vifusi vya majengo yaliyoanguka na wakijaribu kuyafikia maeneo yasiyofikika kwa urahisi. Televisheni ya taifa ya Moroccoilionesha watu wakiwa wamejazana katika mitaa ya Marrakech wakati wa usiku huku wakihofia kurejea kwenye majengo. Katika mji huo, Msikiti maarufu wa Koutoubia uliojengwa karne ya 12, ambao mnara wake una urefu wa mita 69 umeharibiwa pia ingawa kiasi cha hasara bado hakijajulikana.

Soma zaidi: Mamia wafa katika tetemeko la ardhi Morocco

Mkuu wa mji wa Talat N'Yaaqoub, ulio karibu na kitovu cha tetemeko hilo Abderrahim Ait Daoud, aliiambia tovuti ya habari ya 2M ya Morocco  kuwa, nyumba kadhaa zilianguka na kwamba huduma za umeme hazipatikani. Baadhi ya barabara pia hazifanyi kazi katika maeneo mengine. N'Yaaqoub amesema kuwa mamlaka zinafanya kazi ili kusafisha barabara katika eneo la Al Haouz ili kuyaruhusu magari ya kubebea wagonjwa kupita na kupeleka misaada kwa waathiriwa. Hata hivyo ameongeza kuwa, umbali mrefu kati ya vijiji vilivyo kwenye milima unamaanisha kuwa itachukua muda kufahamu kiwango cha uharibifu uliotokana na tetemeko hilo la ardhi.

Raia wakiwa nje baada ya tetemeko la ardhi MoroccoPicha: Fadel Senna/AFP/Getty Images

Jeshi la Morocco na huduma za dharura liliratibu juhudi za kufikisha misaada katika maeneo yaliyopatwa na uharibifu. Awali, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa barabara zinazoelekea kwenye eneo la milima karibu na sehemu iliyoathiriwa zaidi na tetemeko hilo zilikuwa zimesongwa na magari, na zimezuiwa na miamba iliyoanguka na kuziziba hali inayopunguza kasi ya uokoaji. Malori yaliyobeba mablanketi, makoti na taa yalikuwa yakielekea huko.

Dunia yaonesha mshikamano na Morocco kufuatia tetemeko

Baadhi ya viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wametoa pole kwa Morocco kufuatia janga hilo. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X ambao awali ulijulikana kama twitter aliandika kuwa "Ni habari mbaya kutoka Morocco. Tuko pamoja na waathiriwa wa tetemeko katika nyakati hizi ngumu".  Shirika la Ujerumani la msaada wa kiufundi limesema linajiandaa kutoa msaada kama litahitajika kufanya hivyo.

Naye Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi wakati akifungua mkutano wa kilele wa mataifa yanayounda kundi la G20 unaofanyika New Delhi amesema kuwa, wanawaombea nafuu ya haraka majeruhi waliotokana na tetemeko hilo la ardhi na kwamba wako tayari kutoa msaada unaohitajika.

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametoa salamu za rambirambi  kwa Mfalme wa Morocco Mohammed wa sita akisema kuwa nchi yake imeguswa na kuhuzunishwa na maafa hayo. Ametoa pole kwa familia na marafiki wa waathiriwa na kuwatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa.

Waokoaji wakiondoa vifusi vya maporomoko ya majengo baada ya tetemeko MoroccoPicha: Abdelhak Balhaki/Reuters

Kwa upande wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) kuwa "tunasimama na kaka zetu wa Morocco kwa kila namna katika siku hii ngumu." Katika taarifa tofauti, wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki nayo imeandika kuwa Ankara, iko tayari kutoa msaada wa hali na mali kwa Morocco.

Vile vile, Rais wa Ufaransa Emannuel Macron, Joe Biden wa Marekani, Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Kaimu waziri Mkuu wa Uhispania, na Waziri Mkuu wa Uswidi wametoa salamu za pole na kuonesha kusikitishwa kwao na tukio hilo.  Umoja wa Falme za Kiarabu na Taiwan, zimetoa pia ujumbe wa pole kufuatia tetemeko hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW