1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi lauwa maelfu ya watu Uturuki na Syria

6 Februari 2023

Idadi ya waliokufa katika tetemeko kubwa la ardhi Uturuki na Syria, imeongezeka na kufikia watu zaidi ya 2000, huku wengine zaidi wakiaminika kukwama chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

Türkei | Erdbeben Diyarbakir
Picha: IHA agency via AP/picture alliance

Tetemeko hilo kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Ritcher lilipiga katikati mwa Uturuki na Syria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 2000 Miji mingi ya Uturuki iliharibiwa vibaya hasa ile iliyowahifadhi wakimbizi kutoka Syria waliokimbia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka 11.

Mkuu wa shirika la kitaifa la kushughulikia masuala ya matetemeko ya ardhi nchini Syria, Raed Ahmed, ameliita tetemeko la leo kuwa baya na kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika shirika hilo.

Inasemekana zaidi ya watu 900 wamekufa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi Syria huku vifo vya watu wengine zaidi ya 1000 vikiripotiwa Uturuki, hii ikiwa ni kulingana na rais wa taifa hilo Recep Tayyip Erdogan, ambaye namna atakavyoshughulikia janga hili ambalo ni moja ya majanga mabaya kushuhudiwa katika miongo miwili ya utawala wake, kutaelekeza iwapo kutakuwa na nafasi yake ya kuteuliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Mei mwaka huu.

Kwa sasa Erdogan ameomba rasmi msaada kutoka kwa washirika wake wa Jumuiya ya Kujihami NATO, wa kukabiliana na hali baada ya tetemeko hilo la ardhi. Wahudumu wa afya wa dharura, vifaa vya matibabu, na makundi ya waokoaji ni miongoni mwa usaidizi Uturuki iliyouomba kutoka Jumuiya hiyo.

Muda mfupi baada ya ombi hilo, Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilisema makundi ya waokoaji kutoka mataifa 8 ya Ulaya ambayo ni  Bulgaria, Croatia, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, Ugiriki, Uholanzi, Poland na Romania, yatapeleka usaidizi huo.

China pia imesema iko tayari kupeleka misaada ya kiutu kote nchini Uturuki na Syria huku Uingereza ikiamua pia kutuma usaidizi wa matibabu mjini Ankara.

Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson ambaye ombi la nchi yake kuingia katika jumuiya ya NATO linapingwa na Uturiki ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba amesikitika kwa kile kilichotokea Uturuki na Syria na kumuambia Rais Erdogan kwamba taifa lake lipo tayari kusaidia pale litakapoweza.

Mataifa zaidi yatoa msaada kwa Uturuki na Syria

Timu ya waokoaji wakiwatafuta manusura chini ya jengo lililoanguka katika mji wa Diyarbakir Kusini Mashariki mwa UturukiPicha: Mahmut Bozarslan/AP Photo/picture alliance

Kyriakos Mitsotakis, Waziri mkuu wa Ugiriki ambaye nchi yake imekuwa katika mgogoro wa muda mrefu na Uturuki kufuatia masuala ya mipoaka na kitamaduni ameahidi pia msaada kwa taifa hilo jirani.

Jumuiya ya kimataifa yatoa mshikamano kwa Uturuki na Syria

Huku rais Vladimir Putin akiahidi msaada kwa mataifa yote mawili Uturuki na Syria kwa kukabiliwa na janga hilo kubwa.

Kwengineko kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani papa Francis amesikitishwa na majanga hayo yaliyotokea Uturiki na Syria na kutuma salamu zake za kiroho kwa wale wote walioathirika kwa tetemeko hilo kubwa la ardhi katika mataifa hayo mawili.

Chanzo: ap/reuters/afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW