1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaMorocco

Tetemeko la ardhi Morocco: Idadi ya waliokufa yafikia 2,681

Hawa Bihoga
12 Septemba 2023

Idadi ya waliokufa katika tetemeko la ardhi Morocco imefikia 2,681 wakati waokoaji wakikimbizana na muda kupekua vifusi kwa matumaini ya kuwapata watu walionusurika katika tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.8

Tetememko la ardhi Morocco - Waokoaji wakitafuta manusura.
Waokoaji wakipekuwa vifusi kutafuta manusura wa tetemeko la ardhi katika mji wa Talat N'Yaaqoub huko Marrakesh, Morocco, Spetemba 11, 2023.Picha: Said Echarif/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Morocco, watu walionusurika wengi wao wamelala nje kwa usiku wa tatu, nyumba zao zikiwa zimeharabiwa au kugeuka zisizokalika, na idadi ya waliokufa ikifikia 2,497, huku waliojeruhiwa mpaka sasa wakiwa 2,476.

Katika kijiji cha Imgdal, umbali wa kilomita 75 kusini mwa Marrakesh, wanawake na watoto walikusanyika chini ya mahema ya muda yaliyowekwa kando ya barabara na karibu na majengo yaliyoharibiwa, baadhi wakijikusanya karibu na moto wa wazi.

Soma pia: Tetemeko la ardhi lauwa watu 2,122 Morocco

Huku sehemu kubwa ya eneo la tetemeko ikiwa katika maeneo magumu kufikika, athari kamili ya janga hilo bado haijajulikana wazi, na mamlaka haijatoa idadi ya watu ambao hawajulikani walipo. Barabara zilizofungwa au kuzuiliwa miamba zimefanya kuwa vigumu kuyafikia maeneo yalioathiriwa zaidi. Madhara yaliyotokea kwa urithi wa kitamaduni wa Morocco yamekuwa yakijitokeza hatua kwa hatua.

Wakaazi wakipumzika katikati mwa Marrakesh kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini Morocco, Septemba 9, 2023.Picha: Hannah McKay/Reuters

Majengo katika jiji la zamani la Marrakech, ambalo ni Turathi ya Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, yameharibiwa vibaya. Tetemeko hilo pia limeripotiwa kusababisha uharibifu mkubwa kwenye Msikiti muhimu wa kihistoria wa karne ya 12 wa Tinmel, katika eneo la mbali la mlima karibu na kitovu chake.

Lilikuwa tetemeko baya zaidi kuwahi kutokea katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini tangu mwaka 1960, wakati ambapo tetemeko jengine lilikadiriwa kuwaua watu wasiopungua 12,000, na lilikuwa kubwa zaidi tangu alau mwaka 1900, kulingana na idara ya Utafiti wa Jiolojia ya Marekani.

Mwitikio wa polepole wa serikali

Walionusurika wanapambana kupata sehemu za kujihifadhi na vifaa wamekosoa kile wanachokieleza kama mwitikio wa polepole wa serikali.

Soma pia: Tetemeko la ardhi Morocco: Mamia waachwa bila makazi

Morocco imetuma jeshi na imesema inaimarisha timu za utafutaji na uokoaji, kutoa maji ya kunywa na kusambaza chakula, mahema na mablanketi. Hata hivyo, si Mfalme Mohammed VI wala Waziri Mkuu Aziz Akhannouch wamelihutubia taifa tangu maafa hayo.

Katika taarifa ya televisheni siku ya Jumapili, msemaji wa serikali Mustapha Baytas alisema kila juhudi zilikuwa zinafanywa kwenye eneo la tukio, na kuongeza kuwa Mfalme Mohammed alimuagiza waziri mkuu kukutana leo na kamati ya mawaziri ambayo inaandaa mipango ya dharura, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba.

Tetemeko la ardhi Morocco: Juhudi za uokozi zaendelea

01:31

This browser does not support the video element.

Morocco imekubali msaada kutoka Uhispania, Qatar, Uingereza na Umoja wa Falme za Kiarabu. Umoja wa Ulaya umesema unatoa euro milioni 1 za awali kwa mashirika ya misaada yasiyo ya kiserikali ambayo tayari yako nchini Morocco, na ulikuwa unawasiliana na mamlaka ya Morocco kutoa msaada kamili wa ulinzi wa raia wa Umoja wa Ulaya, ikiwa itahitajika.

Soma pia: Idadi ya waliokufa kwa tetemeko Morocco yazidi watu 2,000

Ujerumani na Ufaransa zimepuuza hatua ya Morocco kutochukuwa mara moja msaada wao, huku Ujerumani ikisema hii leo kwamba haiuchukulii uamuzi huo kuwa wa kisiasa, ikijua kutokana na uzoefu wake wa mafuriko mabaya ya mwaka 2021, kwamba uratibu wa misaada ulikuwa muhimu kuepusha waokoaji kuzuwiana.

Ufaransa ilisema jana kuwa iko tayari kusaidia wakati wowote Morocco itakapotoa ombi rasmi, na utata wowote juu ya suala hilo ulikuwa makosa.

Paris na Rabat zimekuwa na uhusiano mgumu katika miaka ya karibuni, hasa kuhusu maeneo yanayozozaniwa, ambayo Morocco inataka Ufaransa iyatambue. Moroccohaijawa na bolozi mjini Paris tangu mwezi Januari.

Chanzo: Mashirika